Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe,akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu kutangaza majina ya Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha tano 2021 Vyuo vya Kati na Ufundi leo June 1,2021 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza majina ya Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha tano 2021 Vyuo vya Kati na Ufundi leo June 1,2021 jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.Gerald Mweli,akitoa ufafanuzi baada ya Waziri wa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu kutangaza majina ya Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha tano 2021 Vyuo vya Kati na Ufundi leo June 1,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu,amesema kuwa Jumla ya Wanafunzi 148,127 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2021,ambapo wasichana 63,878 na wavulana 84249 ya wanafunzi waliofanya mtihani kidato cha nne mwaka 2020.
Hayo ameyasema leo June ,1,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja maafisa elimu mkoa kwa njia ya mtandao ,Mhe.Ummy amesema kuwa hiyo ni baada ya kufanya uchambuzi na kuona kuwa wamekidhi vigezo.
Aidha ameainisha tahasusi za masomo kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano ambapo wanafunzi 41,504 watajiunga kusoma tahasusi za Hisabati na Sayansi na wanafunzi 46,159 watasoma tahasusi za masomo ya sanaa na biashara.
“Muhula wa kwanza wa masomo utaanza Mwezi Julai 5,2021 na atakayechelewa kuripoti watapangiwa wanafunzi wengine”amesema Mhe.Ummy
Matokeo ya Kidato cha Nne 2020 yanaonesha kuwa Watahiniwa wa Shule waliopata Daraja la I – III walikuwa 153,464 wakiwemo wasichana 67,135 na wavulana 86,329 sawa na asilimia 35.06 ya watahiniwa waliofanya mtihani.
“Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani wakiwa chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) waliofaulu kwa Daraja la I – III ni 479 wakiwemo wasichana 289 na wavulana 190”amesema
Idadi hiyo ya wanafunzi wenye sifa imejumuisha wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 288 wakiwemo Wasichana 123 na Wavulana 165.
Aidha, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani wakiwa chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ni 287 wakiwemo wasichana 149 na wavulana 138.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mwaka 2021, ni kutoka Shule za Serikali, zisizo za Serikali, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani wakiwa chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na waliosoma nje ya nchi ambao matokeo yao yamefanyiwa ulinganifu wa Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA).
Jumla ya wanafunzi 87,663 wakiwemo wasichana 41,885 na wavulana 45,778 sawa na asilimia 59.18 ya wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule 476 za Serikali zikiwemo shule mpya 42, Kati yao wanafunzi wenye mahitaji maalumu walikuwa 288 wakiwemo wasichana 123 na wavulana 165 sawa na asilimia 100% ya wenye Mahitaji Maalum waliokuwa na sifa za kujiunga na Kidato cha Tano.
Wanafunzi 1,598 wakiwemo wasichana 592 na wavulana 1,006 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika Vyuo vinne vya Ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Usimamizi wa Maendeleo ya Maji (WDMI) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Jumla ya wanafunzi 55,308 wakiwemo wasichana 21,401 na wavulana 33,907 wamechaguliwa kujiunga kwenye kozi mbalimbali za ngazi ya Astashahada na Stashahada (Certificate and Ordinary Diploma) katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo Wanafunzi 2,235 wakiwemo wasichana 1,162 na wavulana 1,073 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Afya ngazi ya Stashahada.
Waziri Ummy amesema kuwa wanafunzi 5,757 wakiwemo wasichana 2,798 na wavulana 2,959 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ualimu ngazi ya Astashahada ya Elimu Maalum, Awali, Michezo, Msingi na Ualimu wa Shule zinazofundisha kwa kutumia Lugha ya Kiingereza (English Medium).
“ Wanafunzi 1,709 wakiwemo wasichana 737 na wavulana 972 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ualimu ngazi ya Stashahada ya Sayansi, Hesabu na TEHAMA. Vilevile, Wanafunzi 45,607 wakiwemo wasichana 16,704 na wavulana 28,903 wamechaguliwa kujiunga naVyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika Kada mbalimbali.
Waziri Ummy alisema Serikali ya Awamu ya Sita ingependa kuona wanafunzi wote waliochaguliwa kwenda Kidato cha Tano wanajiunga kwa pamoja ndani ya muda uliopangwa.
“Serikali inawahimiza Wanafunzi ambao wameshakata shauri kujiunga na shule za Binafsi kuthibhibitisha kujiunga na shule hizo kupitia mfumo wa “Selform” uliotumika wakati wa kubadilisha tahasusi”amesema .
Aidha Mhe.Ummy amewataka wakuu wa shule za Binafsi ambazo wanafunzi watadhibitisha kujiunga nazo, watatakiwa kuthibitisha kuwatambua wanafunzi hao kupitia mfumo wa “Selform”.
Nafasi zitakazopatikana kwa njia hii zitajazwa na wanafunzi kwenye “Second Selection” ili nao waweze kujiunga na shule kwa muda sawa na wenzao.
Fomu za maelezo ya mahitaji ya kujiunga na Kidato cha Tano (Joining Instructions)
kwa shule zote za Kidato cha Tano zinapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI
kupitia kiunganishi cha www.tamisemi.go.tz. Vilevile, mfumo wa Selform unaendelea kupatikana kupitia anuani ya selform.tamisemi.go.tz.
Amesema kuwa kwa wanafunzi waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wanapaswa kuthibitisha kukubali kujiunga na kozi walizochaguliwa kuanzia tarehe ya leo hadi ifikapo tarehe 8 Agosti, 2021.
Wanafunzi hawa watatakiwa kufanya Uthibitisho kuwa wamekubali Kozi na Vyuo walivyopangiwa kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambayo ni www.nacte.go.tz kupitia kiunganishi kinachoitwa Uthibitisho TAMISEMI.
Kwa mwanafunzi atakayetaka kufanya mabadiliko ya kozi na chuo alichopangiwa ataruhusiwa kufanya hivyo kuanzia tarehe 9 – 23 Agosti, 2021 kupitia tovuti ya
NACTE ya www.nacte.go.tz.
Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwaka, 2021 inapatikana kwenye tovuti ya OR- TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi ya www.nacte.go.tz.
Kwa upande wake Naibu katibu mkuu TAMISEMI Gerlad Mweli alisema zaidi ya shule mpya 10 zimeongezeka hali iliyowezesha wasichana wote kuchaguliwa kuendelea na masomo kidato cha tano