……………………………………………………………………….
Na Farida Saidy, Morogoro.
Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania -TAWA imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa kitalii ili kuongeza uwezo wa kifedha katika kusimamia maeneo yaliyo chini ya Mamlaka hiyo, ikiwa ni moja ya mkakati wa ukuzaji na uendelezaji wa Mamlaka pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Hayo yameelezwa na Kaimu Kamishina wa Uhifadhi wa Wanyamapori nchini Bwana Mabula Misungwi Nyanda wakati akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake ambapo amesema moja ya mkakati wa kuboresha uhifadhi na mapato ya serikali ni kutenga maneo ya uwekezaji wa kitalii ambayo yatatoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika Sekta ya Utalii.
Maeneo hayo ya hifadhi ni pamoja na Mapori ya Akiba Mpanga-Kipengere, Pande, Mkungunero,Kijershi,Swangaswanga na eneo la urithi wa dunia la Kilwa ambalo pia limetenga maeneo maeneo matatu kwa ajili ya uwekezaji ambayo ni Kilwa Kisiwani.Songo Mnara na Sanje Kati.
Aidha kutokana na jitihada zinazofanywa na Mamlaka hiyo katika uhifadhi wa mapori ya akiba zimezidi kuwavutia watalii wengi kuweza kutembelea vivutio vya utalii katika mapori ya akiba,kutoka watalii 35,479 katika kipindi cha mwaka 2015-2016 na kufika watalii 129,428 katika kipindi cha 2018-2019.
Katika hatua nyingine Bwana Misungwi amewataka watanzania kuwekeza katika ufugaji wa wanyamapori kupitia bustani za wanyamapori(wildlife zoos),mashamba (wildlife farms) na ranchi za wanyamapori (wildlife ranches),ambapo mwekezaji anatakiwa kumiliki eneo lake ambalo atafanyia uwekezaji.
Aidha ameongeza kuwa mpaka sasa jumla ya vitalu 28 vimetengwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia biashara ya uwindaji wa kitalii,ambapo mwekezaji hupewa kitalu kwa ajili ya kukitumia katika shughuli ya uwindaji kikiwemo kitalu cha Selous GR MT kilichopo hifadhi ya Selous.
Sambamba na hayo Mamlaka imetenga jumla ya maeneo kumi na mbili kwa ajili ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife investment concession Areas- SWICA) yakiwemo Grumeti,Ikorongo,Maswa Mbono,Maswa Kimali,Mkungumero,Rungwa Inyonga,Selous LL1, Selous MT2, Selous MHJ1, Selous MHJ2, Selous ML1 na Lake Natron East,ambayo yana jumla ya km2 15,149.