Naibu Spika Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma akizungumza na Wassanii juu ya kutumia sanaa katika kufikisha ujumbe na kuibua matatizo yanayoikabili jamii katika hafla ya Ufunguzi wa Filamu ya Salome Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Kampuni ya Manfizzo Dunia Othman akiiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuisimamia filamu ya Salome inayozungumza Ugojwa wa Festula katika Ufunguzi wa Filamu hiyo hafla iliyofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Muwakilishi kutoka Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud Juma akizungumzia kutoa mashirikiano kwa Kampuni ya Manfizzo katika Ufunguzi wa Filamu ya Salome Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Picha Na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
………………………………
Bahati Habibu Maelezo Zanzibar
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma amewataka wasanii kutumia sanaa katika kufikisha ujumbe na kuibua matatizo yanayoikabili jamii.
Ameyasema hayo huko ukumbi wa sanaa uliopo Rahaleo Mjini Zanzibar wakati wa uzinduzi wa filamu ya Salome inayozungumzia ugonjwa wa Festula unaowakumba wanawake waliofikia umri wa kubaleghe.
Amesema sanaa ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe kwa jamii unaotoa mantiki na kufahamika kwa haraka kwa walengwa ili kuondosha matatizo yaliopo katika sehemu husika.
Amesema kwa sasa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mimba na ndoa za utotoni, dawa za kulevya na vitendo vya udhalilishaji hivyo ni vyema wasanii kutumia sanaa zao kueleza athari zinazoikumba jamii kutokana na matatizo hayo.
Akielezea ugonjwa wa Festula amesema imefika wakati kwa wanaume kuacha kuwanyanyapaa wanawake mara baada ya kupata Festula kwa kuwaacha au kuwatelekeza na watoto hali inayopelekea ongezeko la watoto wa mitaani.
Aidha amewataka wananchi kuamini kuwa ugonjwa wa Fistula ni sawa na magonjwa mengine yanayotibika hivyo kuwataka wanawake kukimbilia hospitali badala ya kuwa dhana potofu ugonjwa huo unatokana na kurogwa.
Akizungumzia suala la maadili amewataka wasanii kuandaa kazi zao za sanaa kwa kuzingatia mila na desturi za watanzania badala ya kuiga mila na desturi za nje.
Nae Katibu Mkuu wa Kampuni ya Manfizzo Dunia Othman ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuisimamia filamu ya Salome ili iweze kuwafikia wananchi wa Mjini na Vijijini kupata elimu ya ugonjwa wa Festula ambao umekuwa ukiwakumba wanawake wengi wa Tanzania.