Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Kisarawe mkoani Pwani Joketi Mwegelo akizungumza leo wakati wa sherehe fupi za kukabidhiwa madarasa manne, matundu ya vyoo na ofisi mbili za walimu kutoka Shirika la Plan International . Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Plan International Peter Mwakabale.
Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani (wa tatu kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Plan International Peter Mwakabale(wa pili kulia) wakishangilia jambo wakati wa tukio hilo la halmashauri ya Wilaya hiyo kukabidhiwa madarasa, matundu ya vyoo na ofisi mbili za walimu.Wengine katika picha hiyo ni Meneja Programu wa Shirika hilo, Ruth Kazoka(wa kwanza kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Ester Laiza(wa pili kushoto) , Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Palaka Charles Msanjila (wa tatu kushoto)pamoja na viongozi wengine wa wilaya hiyo.
Mkurugenzi wa Plan International Peter Mwakabale(aliyesimama) akizungumza wakati wa kukabidhi madarasa, matundu ya vyoo pamoja na ofisi mbili za walimu wa Shule ya Msingi Palaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.Wengine katika picha hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo(aliekaa baada ya Mkurugenzi) akiwa na maofisa wa Shirika hilo pamoja na viongozi wengine.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo(wa pili kushoto) akiisoma hotuba yake kabla ya kuitoa kwa wananchi wakati wa tukio hilo la kukabidhiwa madarasa manne, matundu ya vyoo na ofisi mbili za walimu.Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la Plan International Peter Mwakabale(wa tatu kulia). na wa kwanza kushoto ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Pala Charles Msanjila
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Palaka Charles Msanjila akisoma hotuba wakati wa tukio hilo la kukabidhiwa kwa madarasa manne, matundu ya vyoo na ofisi mbili za walimu .
Sehemu ya wananchi wakiwa na baadhi ya walimu kutoka shule mbalimbali za Wilaya ya Kisarawe walioshiriki tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo (wa tano kulia) akiwa na maofisa wa Plan International pamoja na wananchi wakati wa tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo akiwa na maofisa wa Shirika la Plan International alipokuwa akikabidhi vifaa vya michezo vilivyotolewa na shirika hilo kwa baadhi ya shule za msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo akisisitiza jambo mbele ya wananchi wakati wa tukio hilo la kukabidhiwa madarasa manne, matundu ya vyoo na ofisi mbili za walimu.
Baadhi ya maofisa wa Shirika la Plan International wakiwa na viongozi wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakifutilia maelekezo ya Mkuu wa Wilaya Joketi Mwegelo(hayupo pichani).
Sehemu ya muonekano wa madarasa yaliyojengwa na Shirika la Plan International kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe katika Shule ya Msingi Palaka.
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Joketi Mwegelo amewasisitiza wananchi ndani ya Wilaya hiyo kuhakikisha wanawasimamia vema watoto wao ili kuipata elimu ambayo ndio mkombozi wa maisha yao hasa kwa kuzingatia Dunia ya sasa inahitaji watu wenye kuelimika.
Joketi amesema hayo leo wakati Shirika la Plan International likikabidhi majengo ya madarasa, ofisi za walimu, matundu ya vyoo na madawati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe baada ya kuyakamilisha kwa kushirikiana na halmashauri hiyo.
Amesema wakati wadau wakiweka nguvu kwenye elimu, kuna baadhi ya wazazi na walezi kwenye Wilaya hiyo wamekuwa na tabia ya kuzuia watoto wasiende shuleni, jambo ambalo amesema halina tija kwa jamii na hivyo ni muhimu kutambua nafasi ya elimu katika dunia ya sasa.
” Miradi hii ambayo inafanywa kwenye elimu pamoja na ustawi wa jamii inagusa maisha ya wananchi wote..Hata hivyo hatuwezi kuzungumzia ustawi wa mtoto bila kuzungumzia familia, kama kijana hana nidhani nitaangalia mzazi wake kama anayo nidhamu, kama mtoto anatoroka shuleni nitangaalia wazazi wake.
“Kuna maeneo mengine Kisarawe Mwalimu anajitajidi kumfundisha mtoto lakini mzazi anamwambia usiende shule, dunia ya sasa inataka elimu, ni ajabu kwa sasa hivi tuanze kuhubiri umuhimu wa elimu, ukitaka mtoto wako atoboe lazima apelekwe shule, na sio kwenda shule kwa ajili ya takwimu bali iwe na mantiki, lazima wazazi tufuatilie mienondo ya watoto wetu shule,”amesema.
Amesema Serikali imeamua kuondoa vikwazo kwa watoto wote, na ndio maana iliamua kutoa elimu bure, hivyo hakuna sababu ya kupishana na serikali kwani inaonesha njia, inatoa elimu bure wewe unamwambia mtoto asiende shuleni.
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Plan International Tanzania Peter Mwakabale ameeleza shirika hilo limefanikiwa kujenga majengo likishirikiana na na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe yakiwemo madarasa manne, ofisi mbili za walimu, kukarabati madarasa matatu.
Pia kuweka madawati 50 katika madarasa mawili , meza mbili na viti sita kwa ajili ya ofisi katika Shule ya Msingi Palaka ambapo vyote vikiwa na thamani ya Sh.129,737,060.
Ameongeza shirika hilo pia limejenga vyoo vya wanafunzi wa kiume matundu 18 na vyoo vya vya wanafunzi wa kike matundu 22 yakiwa na chumba cha kubadilishia pindi wanapopatwa na dharura na chumba cha watoto wenye ulemavu yenye thamani ya Sh.147,916,938 ikiwa pamoja na ukarabati wa vyoo vya kiume matundu manne Shule ya Msingi Mloganzila B,vyoo vyote vilivyojengwa vimewekewa mfumo wa kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya usafi wa mazingira.
“Mradi huu wa ujenzi umefanyika katika shule zetu nne ambazo ni Palaka ujenzi wa madarasa manne , ujenzi wa ofisi mbili za walimu na ukarabati wa madarasa matatu.Mloganzila ,Maguruwe na Chang’ombe B, vyoo vya watoto wa kike na wa kiume vyote vikiwa na mfumo wa kuvuna maji ya mvua,”amesema Mwakabale.
Aidha amesema wahenga walisema mwenye macho haambiwi tazama, hivyo haaamini kama kuna mtu miongoni mwao ambaye hajui umuhimu wa elimu kwa watoto na kwamba elimu ni kitu muhimu na cha msingi, ambacho hufumbua fikra na kuwafanya kufikiri chanya na kutoka katika wimbi la umasikini.
“Hivyo naamini watoto wetu wakikaa katika mazingira safi wanaweza kusoma vizuri na kufanya vema katika mitihani yao.Ni ukweli usiopinga mazingira yanapokuwa tulivu watoto hupenda kuhudhuria shuleni,””amesema.
Aidha amesema Plan International inafahamu walimu wana changamoto nyingi zinazokwamisha juhudi na ufanisi wao wa kazi katika kupambana na adui ujinga.”Changamoto hizo ni ukosefu wa vitabu, nyumba za walimu, madarasa na vyoo bora.”
Mwisho