Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jJijini Arusha, Tarehe 31 Mei 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal)
Na Mathias Canal, Wizara
ya Kilimo-Arusha
WIZARA ya Kilimo imesema kwa sasa imeweka msukumo kwa
wawekezaji kuzalisha pembejeo hapa nchini ili kurahisisha upatikanaji wake.
Aidha, imeeleza inapambana kutafuta masoko ili bei za
bidhaa mbalimbali za mazao zipande na kuwa zenye tija kwa mkulima.
Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha jana tarehe 30 na
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa
habari ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kupitia hotuba ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan pamoja na maelekezo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Daniel
Chongolo hivi karibuni kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija.
Amebainisha kwa sasa wanaweka msukumo kwa wawekezaji
kuzalisha pembejeo hapa nchini ambapo katika kufanikisha hilo hivi karibuni alitembelea
kiwanda cha mbolea cha Minjingu kuhakikisha kinafanya upanuzi na kuongeza
uzalishaji.
”Kuna kiwanda kingine kinajengwa Dodoma, kuna viwanda
viwili vya viuatilifu vinajengwa hapa Arusha na tunataka kuwahakikishia
wawekezaji hao kwamba tutawapa kipaumbele katika kununua pembejeo,” Amesema
Ameeleza kuwa baadhi ya maeneo matumizi ya mbolea
yanahitaji kuwekwa chokaa ili iweze kuwa na tija katika kilimo hivyo kwa sasa
wanaongeza juhudi za kupima afya ya udongo na aina yake.
Aidha, amesema yatafanyika mafunzo rejea mengi kwa
mabwana shamba ili kutoa ushauri wa matumizi ya mbolea sehemu ambayo inahusika.
Amesema licha ya kutokuwa na shida ya soko la mafuta
nchini kwakuwa ipo ardhi ya kutosha kuotesha alizeti, michikichi, pamba lakini
bado yanaagizwa kutoka nje ya nchi.
”Tunakidhi mahitaji ya mafuta ya kula kwa asilimia 47 tu
nchini na hiyo inatokana na tija ndogo ya uzalishaji kiasi kwamba inakuwa ni
bei rahisi zaidi kuagiza mafuta kutoka Malaysia, Indonesia, kuliko kuchukua
mafuta ya mawese au ya alizeti.
Kwa hiyo suala hapa kubwa ni tija na soko kwenye mafuta
ya kula lipo, kwenye ngano lipo, takribani tani 800,000 mpaka milioni moja humo
ndani tunazalisha tani 77000, soko la ngano lipo, uzalishaji ni mdogo na tija
ni ndogo kiasi kwamba ngano inayokuja kutoka nje inaonekana ni bei ndogo zaidi
kuliko inayotumika hapa nchini,” Amesema.
Ameeleza unaweza kwenda na zao moja hado jingine
ukagundua kuwa changamoto iliyopo ni tija na kwamba wamegundua ili kupambana na
changamoto hiyo ni lazima kufanya utafiti ili kuwa na mbegu bora.
”Sasa kuna mbegu zimegunduliwa pale Kibaha kwenye kituo
cha utafiti ambapo ikitumika kwa hekta moja unaweza ukapata kuanzia tani 22
mpaka 50 za mihogo.
Sasa hivi tunapata wastani wa tani 8 mpaka 3 kwahiyo hata
soko la China ambalo tunataka kupeleka mihogo sasa hivi tunashindwa kufanya
hivyo kukidhi mahitaji ya soko kwa sababu tija ni ndogo”
Ameongeza:”Lakini vilevile, mihogo inazalisha Starch,
tunaagiza Starch toka nje kwa sababu hatujazalisha mihogo ya kutosha kuzalisha
Starch hapa nchini kwa utafiti na mbegu bora tunaweza tukajitegemea kwenye vitu
vingi, Lakini chamngamoto kubwa
kwetu ni pembejeo kwa sababu nyingi zinaagizwa nje na kwa gharama kubwa,”.
Pia Waziri Mkenda amesema kuwa, kunapokuwepo changamoto
ya soko la mazao ni lazima gharama za uzalishaji zitakuwa kubwa na matokeo yake
mkulima halimi kwa faida.
Amesisitiza kuwa kwa sasa wanapambana na masoko kwakuwa
ni suala ambalo lazima walivalie njuga na wanafanya hivyo ili bei ianze kupanda.
”Tunafuatilia bei za mahindi kwa mfano Ruvuma huko, Mbeya
ziko chini sana ukilinganisha na gharamaza uzalishaji,” Amesisitiza
MWISHO