……………………………………………………………………
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa 05 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya mauaji, kujeruhi na kuingiza bidhaa nchini bila kulipia ushuru.
KUKAMATWA MTUHUMIWA WA MATUKIO YA KUJERUHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia FURAHA SHIPINDI [37] mkazi wa DDC – Mbalizi kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kujeruhi.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 28.05.2021 majira ya saa 21:00 usiku huko mtaa wa DDC katika Mji Mdogo wa Mbalizi, Kata ya Utengule, Tarafa ya Usongwe, Mkoa wa Mbeya. Katika upekuzi, mtuhumiwa alikutwa akiwa na shoka dogo, nondo iliyochongwa mbele na begi dogo lenye nguo anazobadilisha kuvaa kila baada ya tukio.
Ni kwamba mnamo tarehe 27.05.2021 huko DDC Mbalizi mtuhumiwa aliwajeruhi watu wawili 1. CHARLES MASINGA [39] Mkazi wa Mlima Reli na 2. PASHAL MSILIKASI [37] Mwalimu wa Shule ya Sekondari Juhudi kwa kuwapiga na kitu butu kichwani. Mtuhumiwa amekiri kufanya matukio hayo na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri hili kukamilika.
KUINGIZA NCHINI BIDHAA BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia PHILIP PETER [49] mfanyabiashara na mkazi wa Jijini Mbeya kwa tuhuma za kuingiza bidhaa nchini bila kulipia ushuru pamoja na kuingiza bidhaa nchini zilizopigwa marufuku.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 28.05.2021 majira ya saa 05:00 alfajiri huko Kijiji cha Bujinga, Kata ya Bagamoyo, Tarafa ya Tukuyu mjini, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya akiwa na Gari yenye namba za usajili T.259 BLA aina ya Toyota Hilux Pickup akiingiza bidhaa mbalimbali nchini akitokea nchini Malawi bila kulipia ushuru ambazo ni:-
- Sukari katoni 30,
- Uyoga mifuko 20,
- Mafuta ya kula ndoo 10 kila moja lita 20,
Aidha mtuhumiwa alikutwa akiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku nchini aina ya Fighter Vodka katoni 60. Taratibu za kiforodha zinaendelea.
KUKAMATWA WATUHUMIWA WA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu [03] ambao ni 1. LUSAJO MWAIJOBELO [32] 2. NABOTI SANGA [44] na 3. CHRISTINA CHAULA [50] wote wakazi wa Kisyosyo – Matema Wilaya ya Kyela kwa tuhuma za tukio la mauaji ya mwanamke aitwaye ELIZABETH MWAIKE [22] Mkazi wa Kisyosyo.
Watuhumiwa wamekamatwa tarehe 28.05.2021 majira ya saa 18:30 jioni huko Kijiji cha Kisyosyo, Kata ya Matema, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya.
Ni kwamba mnamo tarehe 11.05.2021 majira ya saa 08:00 asubuhi huko kwenye machimbo ya Kokoto ya kampuni ya kichina inayojenga kituo cha forodha Kasumulu, Kitongoji cha Lusonjo, Kijiji cha Kisyosyo, Kata ya Matema, Tarafa ya Ntebela,Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. ELIZABETH MWAIKE [22] Mkazi wa Lusonjo – Kisyosyo alikutwa eneo hilo akiwa ameuawa kwa kupigwa kitu kizito kichwani umbali wa mita 500 kutoka nyumbani kwake huku chanzo cha tukio hilo kikielezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
KUKAMATA MALI YA WIZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kukamata mali ya wizi ambayo ni Pikipiki moja aina ya TVS isiyokuwa na namba katika misako inayoendelea maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya dhidi ya uhalifu na wahalifu.
Pikipiki hiyo ilipatikana katika msako uliofanyika tarehe 28.05.2021 majira ya saa 04:00 alfajiri huko Kijiji cha Magea, Kata na Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Msako mkali unaendelea wa kumtafuta mtuhumiwa ambaye aliitelekeza Pikipiki hiyo na kisha kukimbia mara baada ya kuwaona askari.
Pikipiki hiyo iliibwa huko Ilembula Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe na tayari imetambuliwa na mhanga.