……………………………………………………………………..
Na. Angela Msimbira, KAHAMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatumia mapato ya ndani kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Akikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Mji wa Kahama mapema leo hii Mhe. Ummy amesema Serikali kwa sasa agenda yake kuu ni kuhakikisha fedha zinazokusanywa katika Halmashauri zinatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo ili kupunguza changamoto mbalimbali katika jamii.
Mhe. Ummy amesema kuwa Serikali itahakikisha inasimamia ukusanyi na kudhibiti matumizi ya mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuhakikisha kile kinachokusanywa kinaenda kutumika kutatua kero za wananchi katika sekta ya afya, Elimu, Miundombinu ya Barabara na utoaji wa mikopo kwa vijana, walemavu na wanawake nchini.
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali imejiwekea mkakati wa kuhakikisha Halmashauri zinazoweza kukusanya zaidi ya bilioni 5 kwa mwaka zinatakiwa kutenga asilimia 60 ya mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na zile Halmashauri zinazokusanya chini ya bilioni 5 wanatakiwa kutenga asilimia 40 ya mapato yake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia Waziri Ummy amesema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali yaliyotolewa katika Halmashauri ya Mji wa Kahama ambapo wametumia mapato ya ndani kujenga miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Kituo cha afya cha Nyasubi kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 500, Kutenga eneo la ekari 200 kwa ajili ya wajasiriamali wa viwanda vidogo Nzogomela, Ujenzi wa shule ya Sekondari Nyihogo, Ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje Hospitali ya Wilaya ya Kahama na Jengo la Utawala.
Waziri Ummy amehimiza Fedha za mapato ya ndani zihakikishe zinaenda kutatua kero za wananchi hususani katika ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, ununuzi wa madawati, ununuzi wa vitabu , ujenzi wa zahanati , vituo vya afya , vifaa tiba na ujenzi wa miundombinu ya barabara.