…………………………………………………….
Kamanda wa kikosi Cha usalama barabarani Wilbroad Mutafungwa amehitimisha mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva 578 wa bajaji na bodaboda mjini Makambako mkoani Njombe na kisha kutoa msaada wa viakisi mwanga 220 na kofia ngumu(elements) 300 ikiwa ni jitihada za kukabiliana na changamoto ya ajali za barabarani.
Akitoa mafunzo kwa vitendo ya usalama barabarani kwa madereva hao yalioandaliwa na wakutunzi kutoka chuo Cha Wide Mutafungwa amesema bado Kuna kiwango kikubwa Cha Mikasa ya ajali za bodaboda nchini ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa maisha ya binadamu na kwamba wakati umewadia kwa jeshi la polisi kitengo Cha usalama barabarani kwa kushirikiana na wadau kuwekeza katika elimu zaidi kwa watembea kwa mguu ,watumiaji wa vyombo vya moto na vijana wadogo mashuleni ili watumike Kama mabarozi kuelimisha wengine.
Takwimu za ajali za bodaboda zinatisha na kukatisha maisha ya wengi ambapo Kamanda Mutafungwa amesema katika mwaka 2020 January Hadi desemba ajali 404 zimetokea kote nchini na kusababisha vifo 280 na kuacha majeruhi 320 huku katika mwaka 2021 kuanzia januari hadi aprili kumetokea Mikasa ya ajali 124 kote nchini ambapo zimesababisha vifo 74 na majeruhi 113 ambao wamegeuka tegemezi huku wengine kuacha familia zinateseka.
Na kwa mkoa wa Njombe Kamanda huyo amesema 2020 kuanzia januari kulikuwa na ajali 10 za bodaboda ambapo vifo vilikuwa 9 majeruhi 3 ,wakati kwa mwaka 2021 januari hadi aprili kwa mkoa huo zitokea ajali 3 ambazo zimeripotiwa polisi na kusababisha vifo 3 na majeruhi mmoja hivyo Kuna kila sababu ya kuongeza jitihada za mapambano dhidi ya ajali za barabarani
Awali Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe Hamisi Issa amesema kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinasababishwa na mwendokasi na kwamba kitendo Cha madereva 578 wa bodaboda na Bajaji kupokea mafunzo hayo ,jeshi litawatumia baadhi yao kwenda katika maeneo mengine ya mkoa wa Njombe na Tanzania kuelimisha wengine kuzingatia Sheria na kanuni za usalama barabarani.
Issa amesema kwamba Jambo pekee la kutokomeza ajali za barabarani ni kuzingatia sheria na alama kwakuwa familia nyingi zimeathiriwa na ajali.
“Umefika wakati dereva anapoenda kazini analazimika kuacha ATA card na vitu vingine vya msingi kwakuwa anakuwa na mashaka ya kutorudi nyumbani kwasababu ya ajali”alisema Kamanda Hamisi Issa.
Kwa upande wake mfufunzi wa mafunzo ambaye pia ni mkuu wa chuo Cha udereva Cha WIDE Faustine Matina amesema katika mafunzo hayo ya siku 3 wamefundisha udereva wa kujihami,uadilifu,usafi,mahusiano na jeshi la polisi pamoja na Sheria na alama za barabarani hivyo kupitia mafunzo hayo tunaimani ajali zitapungua.
Mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo Matina pia akamuomba Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Tanzania Wilbroad Mutafungwa kumpa nafasi nyingine ya kutoa mafunzo mengine mjini Makambako kwa kuwa Kuna kundi kubwa la madereva ambao hawajapata mafunzo hayo kupatiwa mafunzo mengine.
Kwa upande wao madereva bodaboda akiwemo Yusuph Godfrey ambaye pia ni mwenyekiti wa madereva bodaboda mji wa Makambako amesema mafunzo walioyapata yamewafanya kuwa na uelewa mkubwa wa Sheria na alama za barabarani na kwamba wanakwenda kumaliza kabisa tatizo la ajali.
Mbali na kudhibiti ajali Mwenyekiti huyo amesema kuwa kazi ya bodaboda imetoa ajira kwa vijana wengi ambao zamani walikuwa wanapiga nondo.
Nae Fadhili Makali ambaye ni meneja wa NMB tawi la Makambako ameunga juhudi za jeshi la polisi katika kukabiliana na ajali za barabarani kwa kutoa msaada wa kofia ngumu 30 na kuahidi nyingine kwa madereva bodaboda .
Aidha Makali ametoa Rai kwa madereva bodaboda na Bajaji kufanya kazi yao kwakuzingatia na kwa bidii kubwa huku pia akieleza fursa ya mikopo ya bajaji na bodaboda inayotolewa na Benki hiyo ambayo mkopaji atapaswa kwanza kutoa asilimia 20 ya fedha ili kupatiwa mikopo hiyo.