Mkuu wa shule ya sekondari Angeline Mabula iliyopo kata ya Kiseke Mwalimu Magweiga C. Magabe akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Nsumba juu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa ya shule hiyo
Wajumbe wa halmashauri kuu Nsumba wakikagua ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari Angeline Mabula iliyopo kata ya Kiseke
Diwani wa kata ya Kiseke Mhe Mwevi Ramadhani Mwevi akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu Nsumba wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi tangu kuisha kwa uchaguzi mkuu Oktoba 2020
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kanda ya Buswelu Bi Julieth Peter akizungumza na wajumbe wa kikao cha halmashauri kuu Nsumba, Kiseke wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi
………………………………………………………………………..
Chama Cha Mapinduzi Nsumba wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza kimeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kufuatia miradi yote ya maendeleo ndani ya eneo hilo kutekelezwa kikamilifu, kwa viwango vinavyostahili na kwa gharama nafuu
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa CCM Tawi la Nsumba Ndugu Hassan Rajab Kagimbo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi katika mitaa ya Nsumba, Zenze na Nyabusalu inayosimamiwa na tawi hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kuisha kwa uchaguzi mkuu Oktoba, 2020 ambapo amefafanua kuwa miradi ya urasimishaji makazi, ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme imetekelezwa vizuri
‘… Kwa taarifa hizi zilizowasilishwa kwetu, Niseme kwa pamoja tumeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi tangu chama chetu kuchaguliwa kuingia madarakani, Tutaendelea kuisimamia Serikali kutekeleza tulichokiahidi kwa wananchi …’ Alisema
Aidha Mwenyekiti huyo akawataka wenyeviti wa mitaa anayoisimamia kuhakikisha wanamuunga mkono diwani wa kata hiyo ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi huku akiahidi kuwachukulia hatua wale wote watakaokwamisha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi iliyonadiwa kwa mwaka 2020-2025
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kiseke Mhe Mwevi Ramadhan Mwevi amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa ushirikiano anaompatia katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kata yake ikiwemo mifuko ishirini aliyoitoa kwaajili ya ujenzi wa Zahanati,ujenzi wa kituo cha polisi kwa kutoa matofali yote yanayohitajika, milioni mbili kwaajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara na utatuzi wa changamoto ya upatikanaji wa maji ambapo kupitia Serikali kuu imeahidi kujenga mradi mpya wa maji katika bajeti ya mwaka 2021/2022
Diwani Mhe Mwevi akaongeza kuwa hafurahishwi na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya Sekondari Angeline Mabula iliyopo mtaa wa Zenze kufutia madarasa hayo kuweka nyufa muda mfupi mara baada ya kukamilika kwake huku akishauri kikao hicho kuomba kuhamishwa kwa mkuu wa shule hiyo na yule wa shule ya msingi Juhudi ili kukomesha uzembe katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo
Nae Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kanda ya Buswelu Bi Julieth Peter akashauri viongozi wa CCM na Serikali kuungana pamoja katika kuwatumikia wananchi sanjari na kuwataka kumaliza tofauti zozote kama zipo ili kuondoa makundi ndani ya chama
Akihitimisha mjumbe wa kikao hicho Bi Victoria Gozbert amesema kuwa anaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo uliowasilishwa na watendaji wa Serikali ndani eneo hilo huku akimpongeza mbunge Mhe Dkt Angeline Mabula kwa namna anavyoshiriki katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo sanjari na kuomba wananchi na viongozi kumuunga mkono