Mwenyekiti wa Taasisi ya wakaguzi wa ndani wa bara la Afrika{AFIIA} Emmanuel Johanes akifunga mkutano wao wa saba uliofanyika jijini Arusha.
……………………………………………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Taasisi ya wakaguzi wa ndani wa bara la Afrika {AFIIA} wameadhimia kufanya kazi kwa kutumia viwango vya kimataifa kwa kuacha kutumia mbinu za kizamani kufanya ukaguzi wakati teknolojia imekuwa pamoaja kuboresha utekelezaji wa serikali katika mipango mbalimbali kwa kuzingatia maadili naufanisi ya kufanya kazi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Emmanuel Johanes wakati akifunga mkutano wa 7 wa wakaguzi wa ndani uliofanyika jijini Arusha ambapo alisema kuwa kwa muda wa siki tatu za mkutano huo wamejadili mambo mbalimbali lakini kubwa zaidi ni kuboresha mbinu za wakaguzi wa ndani hasa katika matumizi ya teknolojia
Johanes alisema kuwa wameangalia ni namna gani ambavyo teknolojia mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoka na kuendelea zinawafanya wakaguzi wawe na kazi ngumu ya kuendana na kasi ya mabadiliko ambapo pia wameweza kuangalia agenda ya ufisadi ambayo kwa Afrika ni tatizo kubwa.
“Tumeangalia ni kwa namna gani wakaguzi wanajukumu la kusaidia kuboresha sera mbalimbali za kudhibiti mifumo inayoweza kusababisha kuwepo kwa mianya ya ufisadi ili tuweze kuzisaidia serikali zetu na hatimaye kuiondolea Afrika changamoto hiyo,” Alisema Mwenyekiti wa Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika,Emmanuel Johanes.
Alifafanua kuwa wameona hayo waliyoyainisha kwa sasa ni kipaumbele kwa wakaguzi ambapo wataendelea kuboresha zaidi kama walivyogundua tatizo kubwa ni changamoto ya jinsi wakaguzi wa ndani wanavyofanya kazi na jinsi wakaguzi wa nje wanavyofanya kazi na watazingatia zaidi kuboresha mahusiano yao na kuangalia ni wapi wataweza kushirikiana kwa pamoja kwani lengo lao ni moja la kusaidia serikali zao.
Kwa upande wake meneja wa AFIA Kafaso Milinga ambaye pia ni mtendaji mkuu wa taasisi ya wakaguzi wa ndani Tanzania alisema kuwa katika mkutano huo umeweza kushirikisha wakaguzi kutoka nchi kumi ambao wamefika moja kwa moja katika mkutano huo huku nchi nyingine zikishiriki kwa njia ya mtandao ambapo dhumuni kubwa ni kuhakikisha wanawapa elimu ya kutosha wakaguzi wa ndani, wakurugenzi na wafanya maamuzi mbalimbali ili waweze kutimiza wajibu wao na kuongeza tija katika utendaji.
“Tumeangalia mada mbalimbali zinazowahusu kwenye masuala ya utawala bora, uongozi, Teknolojia ambayo inabadilika kila siku pamoja na masuala mengine yanayowahusu,”Alisema Milinga.
Naye mmoja wa washiriki wa mkutano huo Adam Kisema kutoka mamlaka ya maji Singida alisema kuwa fani ya ukaguzi ni fani ambayo inabadilika kila siku hivyo mkutano huo umewafanya kujiimarisha zaidi ambapo wameweza kubadilishana mawazo.