Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi, Japhet Maselle, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki utakaotumia kadi mara baada ya kuuzindua katika eneo la Kivukoni mkoani Dar es salaam.
Abiria wakitumia mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki utakaotumia kadi katika Kivuko cha Magogoni na Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu.
WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), umezindua mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki utakaotumia kadi katika Kivuko cha Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo uliofanyika tarehe 26 Mei, 2021 katika eneo la Kivukoni, Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, alisema kuwa mfumo wa N-Card utasaidia kupunguza msongamano katika kivuko hicho, kutokana na kwamba unatoa huduma kwa haraka tofauti na mfumo uliokuwa ukitumika awali.
Aidha, alisema kuwa mfumo huo mpya unafanya kazi kwa kutumia teknolojia ambayo inamtaka abiria kuwa na kadi hiyo inayopatikana kwa gharama ya Sh.1000 na baada ya kununua ataweka fedha kupitia wakala wa N-Card au mitandao ya simu kuanzia kiwango cha Sh. 500 na kuendelea.
“Huduma hii inapatikana katika vivuko vyetu vyote vya Magogoni na Kigamboni na juhudi zinaendelea ili kuhakikisha kuwa tunaongeza wigo wa abiria kuweza kujiwekea salio kwa kutumia benki na mitandao ya simu iliyobakia”, alisema Eng. Maselle.
Aliongeza kuwa abiria mwenye kadi yenye salio akifika kivukoni atagusisha kadi yake kwenye geti na kukatwa nauli stahiki ya Sh.200 na hatimaye kuweza kupita.
Amefafanua kuwa zoezi hilo ni la sekunde moja tu kutokana na kuwa na mageti yenye kasi kubwa ya kufungua na kufunga, hivyo kuweza kuhudumia idadi kubwa ya abiria kwa muda mfupi na kuondoa msongamano.
Amebainisha kuwa kwa sasa mifumo yote miwili ya tiketi za karatasi na kadi zitaendelea kutumika hadi hapo mfumo wa kielektroniki utakapozoeleka kwa abiria.
Maselle amefafanua kuwa tangu mfumo huo uanze umeonesha mafanikio makubwa hasa kuondoa tatizo la abiria kupanga foleni mbili ya kununua tiketi na ya kuruhusiwa kuingia eneo la kusubiri kivuko.
TEMESA imesimika mageti mawili pande zote mbili za vivuko na inatarajia kubadilisha mageti yote ya zamani na kuweka mapya ili kurahisisha huduma hiyo kufanyika kwa ufanisi zaidi.
“Napenda kuwatoa hofu wananchi hasa wale ambao ni wageni kuwa mifumo yote miwili itaendelea kutumika hadi hapo usimikaji wa mageti yote utakapokamilika”,amesisitiza Eng. Maselle. .
TEMESA kwa kushirikiana na NIDC itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo huu wa kadi ili kuwaondolea changamoto mbalimbali, elimu itahusisha kujua sehemu ya kupata kadi, kuweka fedha na namna ya kujua salio lililobaki kwenye kadi.
Kufuatia utaratibu huo abiria akipata changamoto yeyote ya kadi anaweza kuwasiliana na watoa huduma waliopo katika vivuko na pia kwa kupiga simu namba 0800 11 01 50 kwa msaada zaidi na huduma hiyo itakuwa bure.