Na Godwin Myovela, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge amekutana na kufanya mazungumzo na wanahabari wote mkoani hapa, ambapo pamoja na mambo mengine, amewaomba ushirikiano wa dhati na kutanguliza uzalendo ili kuweza kusukuma kwa KASI maendeleo ya mkoa
Dkt Mahenge alivunja rekodi hiyo jana kwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kutembelea ofisi za wanahabari mkoani hapa, sambamba na kutumia takribani masaa matatu kusikiliza kero mbalimbali zinazoisibu tasnia hiyo, kwa minajiri ya kupata majawabu kwa umoja na pamoja.
“Nawaomba sana ndugu zangu wanahabari tushirikiane kuijenga Singida yetu, nipo pamoja nanyi, na ofisi ya Mkuu wa Mkoa ipo wazi kama kuna lolote kwa muda wowote karibuni,” alisema Dkt Mahenge na kuongeza;
Singida ni mkoa tajiri sana..una kila kitu, ndio mana nimeanza kukutana na ninyi nikitambua kundi hili ni wadau muhimu sana katika kuhamasisha kasi ya maendeleo tunayoyahitaji kama mkoa,” alisema.
Miongoni mwa kero kubwa aliyokutana nayo mbele ya wanahabari hao ni ukosefu wa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa jengo lake la ofisi ili kukabiliana na kero ya gharama za kupanga, sambamba na tasnia hiyo kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya taasisi zikiwemo za umma, hali inayopelekea kuzorotesha ufanisi wake.
Dkt. Mahenge pia alijulishwa kuhusu urasimu na unyanyapaa wa upatikanaji wa taarifa kutoka kwenye baadhi ya taasisi na idara za serikali, hususani ndani ya halmashauri na Manispaa, huku akitakiwa kuweka mkazo katika jambo hilo.
Aidha, wanahabari hao walimuomba kuwasiliana na mamlaka husika za kiutumishi kuharakisha katika kujaza nafasi ya Afisa Habari na Mawasiliano ndani ya ofisi yake, lengo ni kuboresha kiungo hicho muhimu,-kwa ustawi wa shughuli zote za usimamizi na uratibu wa matukio ya upatikanaji wa taarifa za serikali kwa wepesi baina yake na mkoa.
Suala lingine lililowasilishwa ni kero ya malipo makubwa ya ushuru na ubovu wa miundombinu kwenye masoko ya kimataifa, hususani soko la vitunguu na mifugo mkoani hapa, hali inayopelekea kufifisha mwamko wa biashara husika kwa wadau wa biashara wa kitaifa na kimataifa, sanjari na kuzidi kuchelewesha kasi ya maendeleo ya mkoa.
Aidha, walimshauri Dkt. Mahenge kuwasiliana na Wizara ya Kilimo ili kuangalia uwezekano wa kusogeza karibu ofisi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kwa lengo la kusaidia utafiti na upatikanaji wa kutosha wa mbegu za alizeti ili kuongeza tija na uzalishaji wake, azma kubwa ni kupunguza gharama kwa Taifa kutumia fedha nyingi kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.
“Mbegu za alizeti zenye sifa ya kutoa mafuta mengi zikiwemo zile za Hysan 33 na Jupiter ambazo ni rafiki kwenye viwanda gharama yake ni Kati ya elfu 35 na 40 kwa kilo..katika hili ukifanya tathmini sio rahisi sana mkulima wa kawaida kuweza kumudu.” alisema mmoja wa wadau hao wa habari
Hata hivyo, Dkt. Mahenge akijibu ombi la kiwanja kwa ujenzi wa ofisi za ‘Singida Press Club,’ alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Mulagili kuhakikisha anaanza kushughulikia suala hilo mara moja, huku akiomba apatiwe mrejesho wa utekelezaji wake.
Suala la tija ya uzalishaji wa zao la alizeti, Mkuu wa mkoa alisema jitihada mbalimbali za kuleta ustawi wa zao hilo muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Singida na Tanzania nzima zinaendelea.
“Yote mliyowasilisha hapa ninayachukua na yatakwenda kufanyiwa kazi kwa ustawi na maslahi mapana ya mkoa wetu wa Singida,” alisema Dkt Mahenge.
Dkt Mahenge ambaye hivi karibuni ameapishwa kuwa Mkuu mpya mkoani hapa kuchukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi (mstaafu), leo ataendelea na utambulisho wake kwa kukutana na Viongozi wa Dini, na kisha kesho atakutana na kufanya mazungumzo na wazee wa mkoa wa Singida.