*******************************
Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Mbeya
Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuwataka Watanzania kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Maafisa hao wamefanya mazoezi ya viungo pamoja na kushiriki kucheza mechi ya mpira wa miguu kwa wanaume kati ya mashabiki wa timu ya Simba na Yanga ambapo mchezo huo umefanyika leo Mei 28, 2021 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) Jijini Mbeya na mashabiki wa timu ya Simba waimeibuka kidedea kwa kuwafunga timu ya mashabiki wa Yanga magoli 3-0.
Akizungumzia mchezo huo, Katibu wa Chama cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini (TAGCO) Abdul Njaidi amesema lengo la chama hicho kuandaa mazoezi kama sehemu ya ratiba ya Kikao Kazi hicho ni kuitikia wito wa viongozi wa Kitaifa na amewahimiza maafisa hao kuendelea na mazoezi wakirudi kwenye vituo vyao vya kazi na kuwahamasisha watumishi wengine kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mwandamizi Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF) ambao ni moja wa wadhamikni kwa Kikao Kazi hicho, Sebera Fulgence amesema lengo lao kudhamini michezo kwa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini ni kuwawezesha kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujiepusha na maradhi mara kwa mara.
Aidha, Sebera amewahimiza wafanyakazi wa umma na sekta binafsi kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yanayotokana na kazi pamoja na magongwa yasiyoambukiza.
Naye Afisa Habari kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar Raya Suleiman Abdallah amesema licha ya michezo kuwa ni afya, pia inasidia kuleta utimamu wa mwili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Kikao Kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali mwaka huu kimefanyika Jijini Mbeya kuanzia Mei 24-28, 2021 kimeshirikisha maafisa hao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambacho kilifunguliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa na kufungwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera.