**********************
Mei 27
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
KITUO cha Msaada wa kisheria Kibaha Paralegal Center (KPC) kinatarajia kutoa elimu ya kisheria kwa watu zaidi ya 40,000 katika mji wa Kibaha kwa mwaka huu ,ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wa serikali za mitaa,hali itakayowasaidia kubaini haki zao za msingi .
Hatua hii inakwenda kuwapa ufahamu wananchi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria hivyo kupunguza changamoto za vitendo vya kuvunja sheria hasa migogoro ya ardhi,ukatili wa kijinsia ambapo kwa kipindi cha nyuma watu wengine walikuwa hawajui sheria zinazopigania haki zao .
Katibu wa kituo hicho Dismas Chihwalo alieleza,lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao juu ya masuala ya sheria ni ili waje kuwasaidia wananchi na kuwaelekeza njia za kufuata ili wapate haki zao.
Chihwalo alibainisha , viongozi hao ndiyo watu wa mwanzo kupata taarifa juu ya masuala mbalimbali yanayokwenda kinyume cha sheria kutoka kwa wananchi wanaowaongoza na kituo kinatoa msaada wa kisheria bure kwa watu kwenye uhitaji wakiwemo wanawake.
“Mbali ya kuwajengea uwezo viongozi juu ya masuala ya kisheria,” tunatoa elimu ya sheria na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ili kutatua migogoro ya kisheria kabla ya kufika kwenye vyombo vya kisheria ili kuvipunguzia mzigo vyombo vya kisheria,”alisema Mlenga.
Alisema ,baada ya kuwajengea uwezo viongozi wa kata na mitaa wanatoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi, wanafunzi wa shule ya Sekondari Mwanalugali na shule ya Msingi Tumbi juu ya sheria ya mtoto na makundi ya vikoba kwenye kata ya Tumbi.
“Kutokana na elimu na msaada wa kisheria tunaotoa kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mabadiliko yameanza kutokea ambapo wananchi wamenza kuwa na uelewa juu ya kutoa taarifa za vitendo vya ukiukaji wa sheria,” alisema Chihwalo.
Nae mwenyekiti wa mtaa wa Mwanalugali Deo Rwekaza alisema kuwa mafunzo hayo yanawasaidia ili wananchi wanapofika ofisini kwake wanapokuwa na migogoro wanawaelekeza njia nzuri ya kuwasaidia kutatua changamoto za baadhi ya migogoro.
Rwekaza alieleza, baadhi ya wananchi wanapokuwa na migogoro wanakuwa hawajui nini cha kufanya au hatua za kufuata mara changamoto ya migogoro inapotokea kabla ya kwenda kwenye vyombo vya kisheria ambako serikali inajitahidi kuhakikisha watu wanaishi kwa Amani.