…………………………………………………………….
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Serikali imesema tayari imeanza kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi katika mahakama na katika vyombo vyote vya kutafsiri sheria mbalimbali hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramaganda Kabudi wakati wa kikao kazi cha Wakurugenzi wa Idara na vitendo vya Sheria vya Wizara za Serikali kubainisha hatua zilizofikiwa katika zoezi la kutafsiri sheria katika maeneo yao.
Amesema kisheria mswada wa mabadiliko ya sheria unapopitishwa na Bunge kisha kiudhinishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sheria hiyo huanza kufanya kazi mara moja, hivyo tayari Rais Samia Suluhu Hassan alishaidhinisha sheria hiyo.
“Mwezi February Bunge lilipitisha mswada huo na April 15, 2021 Mhe. Rais iliidhinisha kwa kutia Saini hivyo sheria hiyo tayari imeanza kufanya kazi punde Rais alipoitipisha, hapo, haisubiri Waziri atoe tamko rasmi” amesema Prof. Kabudi.
Aidha amebainisha kuwa sio kwamba Kiswahili kilikuwa hakitumiki katika mahakama bali lugha ya Kiingeleza ndio ilikuwa lugha chaguo la kwanza katika mahakama, lakini sasa Kiswahili ndicho kitakuwa lugha chaguo la kwanza.
Waziri Kabudi amesema kinachoendelea kwa sasa ni kutafsiri sheria zote kuwa katika lugha ya Kiswahili na aliwataka kila Wizara kutafsiri sheria inazozitumia kuwa kwa lugha ya Kiswahili, hivyo leo wamekutana kujadili mwenendo wa kutafsiri ya sheria hizo na changamoto zake.
“Kimsingi sheria imeanza kutumika kama kuna mapungufu yatafanyiwa kazi, sote tunajua hata mtoto akizaliwa huwa haanzi kutembea bila kutambaa, hivyo huanza kutambaa kusimama kwa kuanguka kisha kuanza kutembea taratibu, kwahiyo na sisi ndio tumeanza” amesema.
Amesema Serikali ya awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na hayati Rais Dk. John Magufuli ilikuwa na uamuzi thabiti ya kufanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya msingi na mama katika utoaji haki mahakamani na katika vyombo vya sheria.
Amesema kazi za Wizara hizo ni kusimamia matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sekta ya sheria na utoaji haki, kushiriki katika uendelezaji wa lugha ya Kiswahili na kuratibu matumizi ya lugha ya Kiswahili na inahitajika ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Kazi ya kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili itakuwa endelevu kwani linahitaji umakini na maandalizi ya kutosha, wadau wote wakiwemo wanazuoni, viongozi wa dini kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita kujitathimini katika zoezi na matumizi ya Kiswahili katika utoaji haki,” amesema.
Aidha Waziri Prof. Kabudi ameonekana kukelwa na baadhi ya watumiaji wa Kiswahili kuharibu lafudhi ya Kiswahili katika matamshi, huku akibainisha kuwa yote hayo ni watumiaji kushindwa kutumia maneno ya kwenye kamusi na kupelekea kuharibu lugha adhimu ya Kiswahili.
“Sisi si Wazungumzaji pekee wa Kiswahili, Nchi za Afrika mashariki zote zinazungumza Kiswahili, Madagascar, Comoro, Congo, tumeacha kujifunza Kiswahili sanifu kwa vile tunajua tumezaliwa na Kiswahili na tunakikua sana misamiati mingi,” amesema.
Amesema Kiswahili ni lugha ya taifa kwa hapa nchini, kimataifa na ya ukombozi kwa bara la Afrika ndio maana kimepata uungwaji mkono na mataifa mengi na kuwa Kiswahili ni lugha ya 10 kwa kuzungumzwa zaidi duniani na inayozungumzwa na mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju amesema,Sheria zote zitatafsiriwa na kupata rasimu ya kwanza, na lugha ya Kiswahili kutumika katika vyombo vya utoaji haki itasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi ambao awali lugha ilikuwa kikwazo kwao.