Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na utapiamlo na udumavu kwa watoto kwa kukosa lishe bora, shirika la Save the chidren kupitia mradi wake wa lishe endelevu wameanza kutoa elimu sambamba na kuwawezesha wananchi mifugo ambayo itasaidia kupata lishe bora katika familia.
Mradi wa lishe endelevu unaotekelezwa na Shirika la Save the children kwa ufadhili wa shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID) unawawezesha wananchi kupata mtaji wa ufugaji wa wanyama wadogowadogo wenye virutubisho ambavyo vitasaidia katika ukuaji wa mtoto tangu akiwa mdogo, pia wanafundisha kilimo mchanganyiko kwa makundi ya vyakula.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Kijiji cha chinangali 1 Wilaya ya Chamwino ambapo pia wamegawa sungura 100 kwa Wilaya ya Chamwino meneja mradi wa lishe endelevu kutoka shirika la save the chidren bw. Gidion Muganda amesema kupitia mradi huo shirika linagawa Sungura, vifaranga wa Samaki na vifaranga vya kuku.
“Kupitia mradi huu tunataka kuziwezesha familia kuwa na lishe bora kwa kugawa vifaranga wa kuku, Samaki na sungura tunaamini nyama hii inavirutubisho vingi ambavyo vitawezesha watoto kukua kwa afya,
“tunagawa kwa wananchi wachache kama mtaji ambapo wakizaliana wanawapa mbegu wananchi wengine hivyo tunaamini baada ya mwaka uzao utakuwa mkubwa na kila mwananchi atakuwa na kuwezo wa kupata lishe bora na kipato kupitia Wanyama hao” amesema Muganda.
Amesema kupitia mradi huo wamepanga kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto chini ya miaka 5, kuongeza idadi ya wanawake walio katika umri wa kuzaa kula vyakula vyenye mchanganyiko kwa kiwango kinachokubalika na kuongeza idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6-23 kula vyakula vyenye mchanganyiko sahihi na kwa wakati.
Amesema kupitia mradi wa lishe endelevu utawafikia wanawake 92,572 walio katika umri wa kuzaa, watoto 75, 118 waliochini ya miaka 5 na vijana walio katika rika balehe, ambapo wanatarajia kuimarika kwa utaratibu wa sekta mtambuka katika ngazi za halmashauri na kuboreka kwa afya lishe, malezi ya watoto, usafi wa mazingira na matumizi ya maji safi na salama.
Amesema miongoni mwa kazi wanazofanya ni kuwajengea uwezo watoa huduma za afya kwenye ngazi ya klinik ili waweze kutoa huduma bora za lishe na ushauri nasaha, kutoa mafunzo ya mkoba wa siku 1000 kwa wahudumu wa afya na kutoa mafunzo kwa wanawake vinara zaidi ya 30 kutoka kwenye kata mbalimbali katika mikoa 4.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino bi. Vumilia Nyamoga akizindua mradi huo amewataka wataalam wa mifugo wa halmashauri kuhakikisha kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kiwango cha juu ili kuzikomboa kaya na tatizo la lishe duni.
“Nitoe maelekezo kwa wataalamu wa mifugo wa halmashauri kuhakikisha kwamba mradi huu unafanikiwa, kila mmoja katika eneo lake apange ratiba maalumu ya kuwatembelea wanufaika wa mradi huu ili kuwapatia ushauri wa kitaalamu na ushauri uwe kwa maandishi” amesema bi. Nyamoga.
Ameshukuru mradi huo kutekelezwa katika Wilaya yake na kwamba mradi huo utasaidia familia zitakazonufaika kujiongezea kipato na lishe bora na kuchangia kukuza uchumi wa nchi, na wanaimani watu wengi watanufaika.
Bi Nyamoga ameongeza kuwa “katika utekelezaji wa mradi huu sasa vifaranga 11,600, sungura 390 na vifaranga vya Samaki 6400 vimeshagaiwa kwa wanufaika wa mradi katika halmashauri za Mkoa wa Dodoma na nimeambiwa katika awamu hii wafugaji 86 katika Mkoa wa Dodoma kati ya hao 25 wanatoka katika Wilaya yetu” amesema.