Meneja wa mradi wa SAFT Bwana Nelson Rutabanzibwa akitoa maelezo ya awali kuhusu mpango wa kutoa mafunzo ya kuwalinda watoto kwa walimu Mjini Songea. katikati ni Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Steven Mashauri Ndaki, na kushoto ni Kaimu afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma Mussa Mkoramigwe
Meneja wa mradi wa SAFT Bwana Nelson Rutabanzibwa akitoa mafunzo kwa walimu 60 walioshiriki mafunzo ya namna kuwalinda watoto yaliyoendeshwa na shirika hilo Mjini Songea.
Meneja wa mradi wa SAFT Bwana Nelson Rutabanzibwa akitoa mafunzo kwa walimu 60 walioshiriki mafunzo ya namna kuwalinda watoto yaliyoendeshwa na shirika hilo Mjini Songea.
Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Steven Mashauri Ndaki,akiwa katika picha ya pamoja na walimu 60 walioshiriki mafunzo ya kumlinda mtoto yaliyotolewa na Shirika la SATF mjini Songea.
…………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Songea
TAASISI ya Social Action Trust Fund (SAFT) inayojihusisha kuwasaidia watoto walio katika mazingira magumu kupata elimu,huduma za afya ya msingi kupitia Bima ya Afya ya jamii, imetoa mafunzo ya kumlinda mtoto kwa walimu sitini (60) wa shule za sekondari kutoka mikoa minne ya Lindi,Ruvuma,Mtwara na Njombe.
Meneja wa mradi wa SAFT Bwana Nelson Rutabanzibwa amesema kuwa, wameamua kuja na mpango wa kutoa mafunzo kwa walimu ambao wao ndiyo walezi wa watoto hawa wawapo shuleni ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.
Alisema, taasisi ya SAFT iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Marekani na serikali ya Tanzania mwaka 1998 hadi sasa inafanya kazi kwenye mikoa 16 na Halmashauri 34 za Tnzania, lengo ni kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, kwa kuwawesha kupata elimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari hadi vyuo ikiwemo vyuo vya ufundi, pia SATF inawawezesha watoto kupata huduma ya Afya ya msingi, ulinzi na haki za mtoto na kuziwezesha kiuchumi kaya masikini ziweze kuwapatia mahitaji muhimu watoto hawa.
Mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Songea pia yalihusisha na taasisi mbalimbali kama vile LIWOPAC kutoka Lindi, FAWOPA kutoka Mtwara, JEUMA na SAFINA kutoka Njombe pamoja na GSM kutoka Ruvuma.
Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Steven Mashauri Ndaki, amelipongeza shirika la SATF kwa kuanzisha utaratibu huu wa kutoa elimu ya malezi na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wadogo na kuwataka walimu waliobahatika kushiriki mafunzo hayo kwenda kuifanyia kazi elimu walioipata.
Baadhi ya walimu wameipongea taasisi hiyo kwa kutoa elimu kwa walezi wa watoto hasa wawapo mashule kwani itawasaidia watoto walio kwenye mazingira magumu kupata haki za msingi.
Mwalimu Emmaculat Ngonyani mshiriki kutoka Wilaya ya Nyasa amesema kuwa, kupitia mafunzo hayo amepata faida nyingi ikiwemo namna mtoto anavyopaswa kupewa mahitaji muhimu. Lakini pia kumsaidia kukabiliana na changamoto zinazotokana na rika barehe kama vile mimba za utotoni zinazopelekea watoto kuacha shule
“faida ambazo nimezipata kwenye mafunzo ya leo ni hasa kama ulinzi wa mtoto, kwa kuwa mtoto anahitaji ulinzi, kuheshimiwa, kupewa mahitaji muhimu, lakini pia kutengenezewa mazingira yaliyo salama ili aweze kusoma na kuishi vizuri
na faida nyingine ni matunda ya matokeo ya kile tunachoenda kukifanya huko mashuleni kwetu”alisema.
Mwalimu Yusuph Madande wa shule ya shule ya sekondari Lindi mkoa wa Lindi, amefurahishwa na mafunzo haya kwa kuwa yamempa somo yeye kama mwalimu na mzazi jinsi ya kumsaidia mtoto hasa wa kike anapokuwa kwenye uhitaji pindi wanapovunja ungo.
“ni taasisi chache sana zinatoa mafunzo kwa walimu wa kiume kuhusiana na mtoto wa kike ,hivyo kwa mafunzo haya tuliyoyapata tumejengewa uwezo wa kuwasaidia watoto wa kike hasa pale wanapofikia kwenye siku zao (hedhi), hasa kwa zile shule ambazo hazina walimu wa kike”
Kwa Upande wake Kaimu afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma Mussa Mkoramigwe ameipongeza taasisi hii ya social Action trust fund (SATF) kwa kutoa elimu kwa walimu, namna ambavyo wanatakiwa kuwajibika kwa kuwalea wanafunzi hasa juu ya matunzo ya mtoto na kudhibiti ukatili kwa watoto.
Walimu wa kutoka mikoa ya Lindi, Njombe, Ruvuma pamoja na Mtwara katika halmashauri zinazotekeleza na mradi huu satf wamepata mafunzo ya namna ya kuwalea watoto ambao ni wanafunzi waliopo katika shule za mikoa hiyo minne ili kuwapa walimu elimu juu ya ukatili na mfunzo ya mtoto.
Amewakumbusha walimu hao, kuhakikisha kila shule inakuwa na vilabu ili kuwawezesha wanafunzi kushiriki katika masuala mbalimbali ikiwemo usafi na utunzaji wa mazingira ili kuleta mabadiliko makubwa katika malezi y watoto wa kike na ushauri juu ya hedhi salama.