Nahodha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 ya Ngorongoro Heroes Kelvin John akiwa katika picha ya pamoja na afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Kizito Bahati na mlezi wa kituo cha kukuza vipaji cha Mwanza Football House Francis Felician
Afisa elimu watu wazima Recipitius Masalu Magembe akimkabidhi kikombe nahodha wa timu ya kanda ya Bugogwa iliyoibuka kidedea katika michezo yote ya UMITASHUMTA
Wachezaji wa mpira wa wavu wa timu ya kanda ya Bugogwa wakichuana na timu ya kanda ya Pasiansi
Wachezaji kutoka kanda za Bugogwa, Pasiansi, Kirumba na Buswelu wakichuana wakati wa mashindano ya kukimbiza vijiti
………………………………………………………………………………………………………………
Mashindano ya umoja wa michezo na taaluma kwa shule za msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yamekuwa yakiibua vipaji vipya na kuendeleza vilivyopo nchini kwa kutoa fursa kwa wanafunzi kuonyesha uwezo wao na kukuza ufahamu wa kitaaluma.
Hayo yamebainishwa na Nahodha wa timu ya taifa ya vijana ya chini ya miaka ishirini (U-20) Ngorongoro Heroes Kelvin John wakati wa kuhitimisha mashindano ya michezo mbalimbali kwa shule za msingi yanayojulikana kama UMITASHUMTA kwa manispaa ya Ilemela yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya wavulana Bwiru ambapo nahodha huyo amewataka washiriki wa mashindano hayo kujituma na kuonyesha vipaji vyao kwani kupitia mashindano hayo uwezo wa kitaaluma unaongezeka sanjari na mawakala wa vilabu vikubwa na shule za vipaji wamekuwa wakiyatumia kuchagua wachezaji wenye vipaji na kuwasajiri katika timu zao
‘.. Kupitia mashindano haya mwaka 2018 taifa likanijua, Kikubwa ni kumuomba Mungu, kuwa na nidhamu na kuongeza juhudi kwa kile unachokifanya ..’ Alisema
Aidha nahodha huyo akawahakikishia ushirikiano wachezaji waliochaguliwa kuunda timu ya manispaa ya Ilemela itakayoshiriki mashindano hayo kwa ngazi ya mkoa ili kuifanya manispaa hiyo kuibuka kidedea na kuendelea kuwa kinara wa kuzalisha na kuibua vipaji tegemezi kwa taifa
Kwa upande wake afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Kizito Bahati amefafanua kuwa mashindano ya UMITASHUMTA kwa mwaka huu yalianza kuratibiwa kwa ngazi ya mashule ikihusisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa pete, mpira wa wavu, kurusha mshale, riadha na baadae kuunda timu za kata kabla ya kuunda timu za kanda nne ya Buswelu, Bugogwa, Pasiansi na Kirumba zilizoshindana kwa ngazi ya wilaya ambapo mpaka kuitimishwa kwake timu ya kanda ya Bugogwa ikaibuka kidedea kwa kuongoza michezo yote.
Akihitimisha michezo hiyo afisa elimu watu wazima Recipius Masalu Magembe akaongeza kuwa mashindano ya UMITASHUMTA yamekuwa yakitoa fursa kwa vijana waliomashuleni kuonyesha vipaji vyao hivyo kuwaasa kuitumia vizuri fursa hiyo kwani mbali na kuimarisha afya zao, Michezo kwa sasa ni ajira na inaweza kuwainua kiuchumi.