Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi wizara ya maliasili na utalii Dkt Allan Kijazi ambaye pia ni Katibu mkuu wa wizara hiyo akiongea na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa kikao cha 28 cha baraza la wafanyakazi la wizara hiyo.
Naibu waziri wa wizara ya maliasili na utalii Mhe: Mary Masanja(picha kutoka maktaba)
**********************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Naibu waziri wa wizara ya maliasili na utalii Mary Masanja amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kuwa wasikivu, wabunifu wachapakazi na sio kuwa wadanganyifu kwa kushirikiana na waalifu.
Masanja aliyasema hayo katika risala yake ya kufunga mkutano wa 28 wa baraza la wafanyakazi wa wizara ya maliasili na utalii iliyosomwa na katibu mkuu wa wizara hiyo Dkt Allan Kijazi ambapo alisema kuwa ni vyema wafanyakazi hao wakatekeleza maadhimio waliyokubaliana katika mkutano huo kwa ufanisi na kwa wakati pamoja na kuwa wasikivu, wabunifu na wachapakazi.
“Ni imani yangu kuwa yote mliyoyaadhimia yatatekeleza lakini pia sitegemei kusikia mtumishi yoyote amejihusisha na uhalifu kwa kuwasaidia majangili kufanya ujangili kati hifadhi zetu za wanyamapori na misitu,”Alisema Masanja katika hutuba yake.
Aidha aliwataka wafanyakazi hao kuhakikisha kuwa elimu waliyoipata katika mkutano huo watakaporudi katika maeneo yao ya kazi wakawaelezee watumishi wenzao ili kwa pamoja waweze kufanya kazi kwa kasi inayofanana na kuweza kufikia mafanikio wanayoyatarajia.
Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni katibu mkuu wa wizara hiyo Dkt Allan Kijazi alisema kuwa mkutano walioufanya kwa siku mbili utaweza kuimarisha usimamizi wa maliasili kwani wamejadili agenda mbalimbali pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili na kujua namna ya kuzitatua.
“Tumekubaliana kwamba lazima tuimarishe nidhamu katika kutekeleza majukumu yetu lakini pia tumekubaliana elimu kuendelea kutolewa kwa wafanyakazi wote ili kuimarisha ufanyaji wa kazi na naamini tutayatekeleza kwa ufanisi unahitajika lakini pia kwa wakati,”Alisema Dkt Kijazi.
Aidha alifafanua kuwa pia katika mkutano huo wamepata elimu ya namna ya kuimarisha afya kwa wafanyakazi pamoja na namna ya kusimamia usalama katika maeneo yao ya kazi kwa manufaa yao na nchi kwa ujumla.