**************************
Madereva wa malori yaendayo safari ndefu za mikoani na nje ya nchi wameliomba jeshi la polisi kikosi cha usalama Barabarani kuyatafutia ufumbuzi mapungufu yaliyopo katika barabarani pindi wawapo safarini.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na baadhi ya madereva wa malori wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Safiri salama iliyozinduliwa leo na kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini Wilbrod Mutafungwa uzinduzi uliofanyika katika eneo la Bandari.
Madereva hao kupitia uzinduzi huo wamemuomba Kamanda Mutafungwa kuwezesha uwepo wa utaratibu wa maeneo ya maegesho ya malori kwa ajili ya mapumziko ya madereva pindi wawapo safarini.
Madereva hao akiwemo Dereva Bigirimana Saidi wamewaomba Polisi wa usalama barabarani kuwa na mahusiano mazuri na madereva huku wakiwaomba kutoa elimu zaidi badala ya kuwaandikia tozo za makosa.
Kwa upande wake kamanda wa Kikosi cha usalama Barabarani nchini Wilbrod Mutafungwa amesema serikali na jeshi la polisi usalama Barabarani limeandaa maeneo maalum kwa ajili ya ukaguzi wa malori yaendayo safari ndefu huku akisisitiza na kuwataka askari wa usalama Barabarani kufanya kazi kwa misingi na taratibu zilizowekwa.
Kamanda Mutafungwa pia ametumia nafasi hiyo kuwaasa madereva wa malori waendao safari ndefu kutenga muda wa kupumzika ili kuepuka ajali za barabarani ambapo amefafanua kuwa baadhi ya ajali husababishwa na uchovu wa madereva.
Aidha Kamanda Wilbrod Mutafungwa amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mwaka huu 2021 mpaka Mei 25 ,2021 zimetokea ajali 81 Tanzania Bara , Majeruhi wakiwa ni 66 na watu 47 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani zilizosababishwa na sababu mbalimbali ikiwomo sababu za kibinadamu.