………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha majanga mbalimbali hasa ya mafuriko na ukame kutokana na uharibifu wa mazingira, serikali imesema inatarajia kuja na kampeni kubwa ya utunzaji wa mazingira ambayo itafanyika nchi nzima kwa makundi mbalimbali na mtu mmoja mmoja.
Hayo yamesemwa leo Mei 24,2021 jijini Dodoma na Waziri ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo amesema katika kusherekea kilele cha wiki ya mazingira Duniani ambayo itafanyika Juni 5 mwaka huu wanatarajia kuzindua kampeni kubwa na ya kihistoria ya utunzaji wa mazingira itakayofanyika nchi nzima.
“Kwa sasa tumeona mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mbali mbali tumeona kule Kigoma maeneo ya ufukweni hayatumiki kabisa, na wanaofahamu kule Mwanza Hotel ya Malaika iliyopo ufukweni baadhi ya maeneo hayatumiki, tumeona hat akule Zanzibar baadhi ya visiwa vimeanza kumezwa, sio hapa nchini tu hata nchi jirani” amesema Waziri Jafo.
Amesema kutokana na hayo wameandaa kampeni kubwa ambayo sasa itakwenda kufanyika ikiwa ni suluhu ya kuhakikisha hali inarejea katika hali yake na itakuwa na kauli mbiu ya “mazingira yangu, Tanzania yangu, naipenda daima” ambayo itafanyika nchi nzima kikamilifu katika maeneo yote.
Katika kilele cha siku ya mazingira Duniani tutazindua kampeni hii na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira June 5 mwaka huu mkoani Dodoma.
Waziri Jafo amesema, kampeni hiyo ya Mazingira kwa Mwaka huu itahusisha kila Idara, zikiwemo Taasisi, Mikoa pamoja na Wilaya, kata vijiji na Mitaaa,Viwanda migodi na maeneo mbalimbali wakiwemo wadau wa usafi na itaungana na utoaji wa tuzo mbalimbali
“Katika hili tutawashirikisha pia washindi wa uandishi wa habari za mazingira ili kuwapa motisha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha jamii hususani watu wa pembezoni wanaelewa umuhimu wa utunzani wa mazingira,”amesema.
Hata hivyo Waziri Jafo amesema anatarajia kukutana na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayohusika na mazingira mnamo mei27 Jijini Dodoma kwa lengo la kuiwezesha kampeni hiyo Jafo amesema kutokana na hayo Ofisi hiyo imewateua wajumbe14 washauri pamoja na mabalozi 40 wa kampeni ya Mazingira lengo likiwa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi shindani kwa kutunza Mazingira.
Aidha amesema, wajumbe 14 ambao amewateua kushauri mwendo wa kampeni,uteuzi wa majaji ili kuhakikisha kampeni inapata mafanikio makubwa amewataja wajumbe hao kuwa ni pamoja na Seif Ally Seif Mkurugenzi wa Superdoll ambaye ni Mwenyekiti, Andrew Komba ni Katibu anatoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dosantos Silayo Kamishina wa TFS .
Pamoja na Mambo mengine amewataja mabalozi 40 aliowateua wakiwemo wasanii pamoja na waandishi wa habari ambapo wote kwa pamoja watahamasisha utunzaji wa mazingira baadhi yao ni Sakina Abdulmasoud ,Oliver Nyeriga,Haji Manara, Antonio Nugaz, Millard Ayo, Diamond, Beka Flauvor, Idris Sulutan, Masoud Kipanya, Christina Shusho, Ester Matiko, Masanja Mkandamizaji na wengine wengi.