Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, akizungumzia maonyesho ya 16 ya shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) ya kanda ya kaskazini, yatakayofanyika kwa siku tatu mjini Babati, kushoto ni Meneja wa SIDO wa Mkoa huo Abel Mapunda.
Meneja wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini (SIDO) Mkoa wa Manyara, Abel Mapunda, akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere (katikati) juu ya maonyesho ya 16 ya Kanda ya kaskazini yatakayofanyika Mjini Babati, kulia ni Ofisa habari wa Mkoa huo, Haji Msovu.
***********************************
Na Mwandishi wetu, Babati
MAONYESHO ya 16 ya kanda ya kaskazini ya Shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini SIDO, yanatarajia kufanyika kwa siku tatu Mjini Babati Mkoani Manyara huku yakihusisha nchi nne za Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Babati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amesema maonyesho hayo yatakayoanza Mei 27 hadi Mei 31 mwaka huu, yatahusisha pia nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.
Makongoro amesema maonyesho hayo yatafunguliwa rasmi Mei 28 na Waziri wa Viwanda na Biashara Kitila Mkumbo na kufungwa naye mkuu huyo wa mkoa Mei 31.
“Pia taasisi mbalimbali nchini zinazohudumia wajasiriamali zitakuwepo wakiwemo TRA, TBS, Brella, NMB, CRDB, NBC, TPB na Azania benki,” amesema Makongoro.
Meneja wa Sido mkoani Manyara, Abel Mapunda amesema kauli mbiu ya maonyesho hayo ni maendeleo ya viwanda nuru ya mafanikio kiuchumi.
Mapunda amesema kupitia maonyesho hayo wananchi watapata fursa ya kujifunza shughuli zinazofanywa na taasisi zinazohudumia wajasiriamali.
“Maonyesho haya siyo kwa ajili ya wajasiriamali pekee hata wananchi wanakaribishwa kutembelea mabanda katika uwanja wa Kwaraa ili kujionea bidhaa na teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa Tanzania,” amesema Mapunda.