Mhe Mbunge wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara mhandisi Samwel Hhayuma Xaday akisalimiana na Katibu mwenezi wa CCM Wilayani Hanang’ Rogathe, baada ya kuchangia matofali 1,000 na lori nne za mchanga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM wa Wilaya hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Hanang’ Yohani Leonce.
…………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara , mhe mhandisi Samwel Xaday Hhayuma amejitolea matofali 1,000 na lori nne za mchanga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya huyo.
Mhandisi Hhayuma amesema amejitolea matofali hayo 1,000 na lori nne za mchanga ili kuwaunga mkono vijana katika ujenzi wa nyumba hiyo ya katibu wao.
Amesema anatarajia hadi mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu nyumba hiyo itakuwa imekamilika na katibu wa UVCCM Hanang’ atahamia.
Amesema endapo nyumba hiyo ikikamilika itampunguzia makali ya maisha katibu wa UVCCM kwani ataepuka kupangisha.
“Nawaahidi kuendelea kuwaunga mkono kwenye ujenzi huu na endapo kutakuwa na changamoto yoyote tuwasiliane,” amesema mhandisi Hhayuma.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Hanang’ Yohani Leonce amemshukuru mbunge huyo kwa kitendo hicho cha kujitolea kuwaunga mkono kwenye ujenzi huo wa nyumba ya katibu wao wa Wilaya.
“Tunakupongeza kwa moyo ulionao mheshimiwa mbunge wetu kwani matofali 1,000 na lori nne za mchanga kwa namba moja au nyingine zitatufikisha mbali kwa niaba ya UVCCM Hanang’ tunakushukuru mno,” amesema Leonce.
Amemuhakikishia mbunge huyo ushirikiano kwa wakati wowote katika jitihada za kujenga Jimbo hilo na Hanang’ mpya aliyoikusudia.
Hata hivyo, amewaomba wadau wengine wajitokeze kuchangia ujenzi wa nyumba hiyo ili ikamilike na UVCCM watakuwa wamepiga hatua moja mbele zaidi.
Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi na wanachama mbalimbali wa UVCCM wakiwemo makatibu wa UVCCM wa baadhi ya kata.
Gharama za matofali hayo 1,000 na lori hizo nne za mchanga ni thamani ya shilingi 1,730,000.