………………………………………………………..
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imekuwa ikipokea malalamiko mengi kuhusiana na vitendo vya rushwa katika sekta ya ardhi. Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 15 ya malalamiko yaliyopokelewa kuanzia Julai, 2019 hadi sasa yanahusu sekta ya ardhi.
Aidha, wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia utendaji wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata kwamba yamekuwa na utendaji unaoashiria vitendo vya rushwa. Tumefanya juhudi mbalimbali za kuondoa rushwa ikiwemo kuchambua mfumo wa utendaji wa Mabaraza hayo na kushauri njia sahihi za kuondokana na mianya ya rushwa, pamoja na kuelimisha wajumbe wa Mabaraza na tumehamasisha wananchi kutupa taarifa pale wanapokutana na mazingira yanayoashiria vitendo vya rushwa wakati wakipatiwa huduma kwenye Mabaraza husika.
Mbali na jitihada hizo, tarehe 16 Mei, 2021 TAKUKURU Wilaya ya Kongwa ilipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja kutoka Kijiji cha Vihingo Kata ya Chiwe Wilaya ya Kongwa kwamba ameombwa rushwa ya shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000/=) ili apewe upendeleo katika shauri lililopo Baraza la Ardhi Kata ya Chiwe. Uchunguzi wetu wa awali ulionyesha ni kweli kuna shauri la mgogoro wa ardhi linaloendelea katika Baraza hilo kati ya mtoa taarifa wetu na mwananchi mwingine.
Pia baada ya kujiridhisha kwamba Bw. Sebastian Albert Ally (31) ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Chiwe alishawishi rushwa hiyo akidai ni kwa niaba ya Bw. Lameck Kamota Chimais (34) ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Moleti na Katibu wa Baraza hilo, na kwakuwa tayari watuhumiwa walishapokea shilingi laki moja (100,000/=) kabla ya hapo, TAKUKURU Wilaya ya Kongwa iliandaa mtego na majira ya saa nne asubuhi ya Jumatatu tarehe 17 Mei, 2021 tuliwakamata Bw. Chimais akiwa ameficha fedha za mtego shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwenye soksi baada ya kupewa na Bw. Ally aliyezipokea kutoka kwa mtoa taarifa wetu.
Wakati TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ilitoa dhamana kwa watuhumiwa wote wawili na Ijumaa tarehe 21 Mei, 2021 walitakiwa kuripoti katika Ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Kongwa lakini alifika Bw. Chimais pekee ambaye siku hiyo hiyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Kongwa na kufunguliwa Shauri la Jinai Namba 56/2021 akishtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo ya mwaka 2019.
Mahakama pia ilitoa hati ya kumwita Mahakamani hapo Bw. Ally na tayari juhudi za TAKUKURU zimewezesha kumkamata jana majira ya alasiri na atafikishwa Mahakamani wiki ijayo.
Tunaendelea kuwasihi wananchi kukataa kununua haki zao na kuwataka kutuletea taarifa za vitendo vya rushwa ili tuzifanyie kazi.
Aidha, TAKUKURU mkoa wa Dodoma inaendela na uchunguzi unaohusu makosa ya ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo ya 2019 dhidi ya Bw. Lyato Tungaraza Bihemo wa Jijini DSM. Ufuatiliaji wetu umebaini kwamba Mtajwa amelipwa na Kampuni za Vodacom na HTT Infranco LTD jumla ya shilingi milioni hamsini na tisa mia tatu thelathini na nne elfu (59,334,000/=) yakiwa ni malipo ya kukodisha eneo la kuweka mnara, ilihali uchunguzi wetu umeonyesha kwamba eneo ulipo mnara huo ni msitu wa hifadhi wa Isabe uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na
hivyo fedha hizo zingepaswa kulipwa kwa Kijiji au Halmashauri hiyo na si kwa Bw. Bihemo.
Uchunguzi umeonyesha pia kwamba mtuhumiwa alifunga mkataba wa ukodishaji wa eneo hilo na kampuni ya Vodacom mwaka 2009 kwa kipindi cha miaka kumi kwa kujifanya kuwa mmiliki halali wa eneo husika na hivyo kwa udanganyifu akajipatia fedha hizo. Tunamtaka Bw. Bihemo kuripoti katika Ofisi zetu mahali popote hapa nchini ili apate nafasi ya kusikilizwa.
Mwisho, tunawakumbusha wananchi wa mkoa wa Dodoma kuwa mtoa na mpokea rushwa wote wana makosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2019, hivyo wale wote wanaopigiwa simu na watu wanaojifanya kuwa ni Maafisa wa TAKUKURU na wanakubali kuwatumia fedha badala ya kutoa taarifa za matapeli hao, nao wanakuwa wametenda kosa la jinai na iwapo tutawabaini hatua stahiki zitachukuliwa pia dhidi yao. Ni vyema kutoa taarifa za Matapeli hao kwenye Ofisi yoyote ya TAKUKURU iliyopo katika kila mkoa na wilaya Tanzania Bara au katika kituo chochote cha Polisi. RUSHWA HAILIPI.