Baadhi ya wadau mbalimbali na wanachama wa mtandao wa Elimu, Washirika wa Maendeleo pamoja na wadau wengine wakishiriki katika mkutano huo. |
Wadau mbalimbali wakishiriki katika mkutano huo wa Elimu Bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET). |
Mmoja wa wadau wa elimu akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET). |
Akizungumza katika mjadala kwenye mkutano wa kimataifa wa elimu Bora, Mkurugenzi Mtendaji Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla alisema kumekuwepo na mjadala mkubwa juu ya elimu inayotakiwa, hivyo kushauri ipo haja ya elimu ya sasa iendane na karne ya 21. “…Tunataka elimu itakayo waandaa watoto wafahamu mambo ya sayansi, wafahamu mambo ya teknolojia, lakini pia wapate zile stadi za maisha. Zipo stadi za kufikiri kwa makini, kuwa wabunifu, kuweza kufanya maamuzi ya busara, kuweza kufanya mawasiliano na wenzao na hata mahusiano yenye tija na si potofu, kutambua jambo hili ni nzuri au baya,” alipendekeza Mkurugenzi huyi ambaye pia ni mwanachama wa TEN/MET.
Alisema Tanzania kwa sasa inaitaji elimu inayoweza kuwatanua vijana ki-fikra, waweze kutenda mambo mbalimbali wamalizapo masomo yao na si kuwaandaa vijana kutegemea kuajiriwa tu. “…Tujaribu kuipitia mitaala yetu kwa makini na kuangalia tuongeze nini, pia tunachotaka kiongezwe kwenye mitaala tukifanyie utafiti, tuhusishea wadau mbalimbali ili kuweza kuibuka na mabadiliko muhimu na sahihi kwenye mitaala hiyo,” alisisitiza Bi. Mgalla.
“…Wadau kama wazazi wanaweza kuulizwa wanataka watoto wao wakimaliza shule waweze kufanya nini, wadau kama mashirika na asasi nazo ziseme zinashauri kitu gani. Mfano sisi tuliosoma zamani tulifundishwa kitu kinaitwa maarifa ya nyumbani, tulijifunza kupika vitu mbalimbali, tulijifunza kushona, tulijifunza kutengeneza bustani, tulijifunza malezi ya watoto na vitu anuai…mambo kama haya tunaweza kuangalia ni yepi tuyarejeshe katika mitaala yetu na kwa namna gani yanaweza kuwasaidia vijana.”
Naye Meneja wa Programu, Nicodemus Shauri kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) alisema kwa sasa nchi yetu inaitaji elimu inayotufaa kuweza kutatua changamoto zinazotukabili, alisema elimu wanayopokea vijana wetu kwa sasa inatakiwa kumjenga na kumuwezesha na hata kumuendeleza kwa karama aliyonayo kijana yoyote ili imsaidie hata kumkwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa kwa namna nyingine watoto wetu wanaweza kupewa elimu huku wakiendelezwa vipawa mbalimbali walivyojaliwa na Mungu ili vije kuwasaidia hapo baadaye. Mfano kama mtu amejaliwa kipaji cha sanaa apate elimu huku akiendelezwa kipaji chake ili baadaye kumuwezeshe kiuchumi, kama amejaliwa historia aendelezwe ili baadaye aje kuwa mwalimu mzuri wa historia, kama amejaliwa kipaji cha muziki aendelezwe ili akitoka shule aje kufanya muziki vizuri utakao msaidia katika maisha yake na kama mtu amejaliwa kipaji cha michezo (mfano riadha au uigizaji) basi aendelezwe ili baadaye imsaidie kwenye maisha yake,” alisema Bw. Shauri.
Alisema vijana wakipewa elimu huku wakiendelezwa kwenye vipaji vyao hawawezi kumaliza shule na kusubiri au kutegemea ajira ambazo kwa sasa ni changamoto ya ki-ulimwengu jambo ambalo litaipunguzia taifa mzigo na kujikuta limewawezesha vijana kiuchumi mmoja mmoja na hata taifa ki ujumla. Alisema kwa sasa tunazungumzia elimu bora lakini pamoja na mambo mengine tuangalie elimu inayotufaa na kujikuta inatukwamua katika changamoto zilizopo.
Kwa upande wake mdau mwingine wa elimu, Bw. Doglas Mwisaka ambaye kitaaluma ni mwalimu alisema licha ya kuzungumzia elimu bora hatuna budi kuwakumbuka walimu ambao ndio wanaokwenda kutoa elimu hiyo, kwamba wanaandaliwa vya kutosha kwa kuzingatia vigezo vyote ili waweze kuifanya kazi hiyo kiufasaha.
“…Tunazungumzia mabadiliko ya elimu kutaka elimu bora, lakini tusisahau kuanza na walimu kwani ndio wadau muhimu wa mabadiliko hayo…siku zote tunafanya maboresho huku mwalimu akibaki nyuma sasa tutapataje elimu bora huku tukiwasahau walimu wenyewe,” alihoji Mwalimu Mwisaka akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mijadala mbalimbali katika Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET). |