*********************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Halmashauri ya jiji la Arusha imeanza mchakato wa kujenga jengo jipya la utawala la ghorofa 6 linalokadiriwa kugharimu bilioni 4 hadi 6 ambalo litajengwa kwa awamu tatu hadi kukamilika.
Akiongea na waandishi habari mkurugenzi wa jiji hilo Dkt John Pima wameshapata fedha kwaajili ya ujenzi huo ambao utawafanya wananchi kuhudumiwa sehemu moja tofauti na ilivyo sasa kwa wananchi kupata huduma kutoka kwa watumishi walio katika sehemu mbalimbali kutokana na ufinyu wa ofisi zao.
“Jengo hili litatoa taswira nzima ya jiji la Arusha ambapo fedha hizo zimetoka serikali kuu huku halmashauri ikichangia asilimia ndogo katika ujenzi huu na tunatarajia litakamilika mwaka 2023,” Alisema Dkt Pima.
Aidha alifafanua kuwa pia kuwa katika baraza hilo watumishi 4600 wameingizwa kwenye utekelezaji wa agizo la Mhe.Rais Samia Suhulu lililotaka watumishi wenye sifa kupandishwa vyeo baada ya kujiendeleza kielimu pamoja na kupewa stahiki mbalimbali ambapo watumishi wapatao 400 wamepewa promotion,watumishi zaidi ya 33 wakibadilishiwa vyeo huku idadi iliyobaki wakirudishwa kazini.
Dkt Pima alisema agizo hilo lilitolewa na Mhe.Rais katika sherehe za Mei Mosi kuwa tangu mwaka wa fedha wa 2018/19 na mwaka 2019/20 hadi kufikia mwaka 2021 watumishi wote wa serikali waliokuwa wanastahili kubadilishiwa vyeo na wengine vyeo vyao kupanda pamoja na kupewa stahiki mbalimbali wapewe.
Alifafanua kuwa jiji la Arusha limetimiza agizo hilo ambapo katika baraza la madiwani watumishi ambao mamlaka yao ya nidhamu iko chini ya baraza ndiyo waliojadiliwa na zaidi ya walimu 3800 wamepata promotion huku wengine wakihamishwa kutoka kwenye kada mbalimbali na kupelekwa katika hatua nyingine.
“Kuanzia sasa hawa watumishi wanasubiri taratibu za kiserikali ili kuweza kupata stahiki zao kama ambavyo Mhe.Rais aliona jambo hilo nila msingi na akaagiza lifanyike.”Alisema Dkt.Pima