Home Mchanganyiko TBA YATOA SIKU 3 KWA WALIOKUWA WABUNGE KUREJESHA NYUMBA ZA SERIKALI WANAZOISHI

TBA YATOA SIKU 3 KWA WALIOKUWA WABUNGE KUREJESHA NYUMBA ZA SERIKALI WANAZOISHI

0

Kaimu Mtendaji Mkuu TBA, Bw.Said Mndeme akizungumza na waandishi wa habari leo  Jijini Dar es Salaam

*********************************

NA EMMANUEL MBATILO

Wakala wa Majengo nchini TBA imetoa siku tatu kwa waliokuwa wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kurejesha haraka nyumba za Serikali wanazoishi Jijini Dodoma huku ikiahidi kuchukua hatua za kisheria endapo watakiuka agizo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mtendaji Mkuu TBA, Bw.Said Mndeme amesema hawatosita kutumia nguvu kuwahamisha Wabunge hao wa Zamani kwani tayari wamepoteza sifa za kuendelea kuishi katika Nyumba hizo.

“Wabunge waliobaki kwasasa ni saba tu ambao  hawajakabidhi nyumba za serikali ambazo wanapaswa kuzirejesha kwetu”.  Amesema Bw.Mndeme.

Aidha Bw.Mndeme amesema mpaka sasa wameshawaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba za serikali katika mikoa ya Mwanza,Arusha, Lindi, Mtwara, Morogoro, Mbeya, Tanga, Iringa na Kilimanjaro wamefanya hivyo kuhakikisha wanaondoa madeni ya kodi za pango katika nyumba za serikali ambazo zinasimamiwa na TBA.

Amesema kuwa kipindi cha miezi minne TBA imekusanya zaidi ya Shilingi bilioni Moja kutoka kwa wadaiwa mbalimbali huku ikiwashauri wadaiwa wengine kulipa kwa kutumia simu zao za Mkononi endapo watashindwa kwenda katika Ofisi zao.