*******************************
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Meja Jenerali John Julius Mbungo, leo Ijumaa Mei 21, 2021 amekabidhi rasmi ofisi kwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za TAKUKURU zilizoko PCCB HOUSE Upanga Dar Es Salaam na kushuhudiwa na na baadhi ya Wakurugenzi wa Taasisi hiyo.
Akizungumza na viongozi pamoja na watumishi baada ya makabidhiano hayo, Meja Jenerali Mbungo amesema anashukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka kwa viongozi na watumishi wa
TAKUKURU kwa kipindi cha miaka minne (2016–2021) alichokuwa katika taasisi hii na kwamba ushirikiano huo ndiyo uliomwezesha kuondoka TAKUKURU akiwa salama.
Kwa upande wake, baada ya kukabidhiwa ofisi, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema mafanikio ya Taasisi hii yatategemea ushirikiano kutoka kwa kila mtumishi. Amesema yeye ni mgeni TAKUKURU lakini si mgeni katika kushughulikia masuala ya mapambano dhidi ya Rushwa kwani anatokea katika Jeshi la Polisi – chombo ambacho kinahusika na usimamizi wa sheria ikiwa ni pamoja na sheria inayosimamia makosa ya rushwa, hivyo hajaanza leo mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha kuwa TAKUKURU inajielekeza katika kutekeleza majukumu ya msingi ya kuanzishwa kwa taasisi hii kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 ikisomwa pamoja na sheria nyingine zinazohusu makosa ya ubadhirifu na uhujumu uchumi.
Vilevile amewataka watumishi wa TAKUKURU kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za utendaji kazi zilizowekwa ili kufikia malengo ya Taasisi na Serikali kwa ujumla.