………………………………………………………………………………
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi CCM taifa Daniel Chongolo amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kubadili mitazamo yao na kujielekeza katika kutatua kero za wananchi waliokipa ridhaa chama hicho kuongoza nchini, badala ya kujadili mambo yasiyokuwa na maendeleo.
Katibu Mkuu Chongolo ametoa wito huo leo mei 21, 2021 wakati walipofika katika ofisi ya CCM Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kujitambulisha wanapoanza majukumu yao mapya akiwa ameongozana na sekretarieti yake.
Amesema CCM si chama za kuzalisha maneno bali ni chama ambacho kimejikita katika kushughulikia kero za wananchi na kusukuma gurudumu la maendeleo kwa wananchi ambao walikiamini chama hicho na kukichagua.
“Hiki sio kiwanda cha kuzalisha maneno nataka kiwe kiwanda cha kuzalisha bidhaa za maendeleo, tusikae kumjadili mtu fulani tukae kujadili kero za wananchi waliotuchagua walituamini ili tuwaletee maendeleo” amesema Chongolo.
Amesema katika uongozi wake watajikita katika kuimarisha mashina ambapo ndio wanapopatikana wanachama wa CCM na ndiko kwenye hazina kubwa na uhai wa chama huku akiwasisitiza viongozi wa mashina kuongeza kasi ya kuwapata wanachama.
Amesema Mkoa wa Dodoma kuwa ndio makao makuu ya nchi ambapo ametaka Mkoa huo uwe mfano kwa mikoa mingine kwa kuwa mkoa huo ndio unaviongozi wote wa chama na serikali hivyo ni lazima uwe na maendeleo katika nyanja zote.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi CCM bara Bi. Christina Mndeme amewataka viongozi katika ngazi zote kufanya kazi kwa kushirikiana na kila kamati ya siasa katika ngazi yake ahakikishe anasimamia miradi ya serikali iliyopo katika eneo lake na kuhakikisha inakamilika kwa viwango na wakati.
“sote tumeona Rais wetu amefungua ushirikiano na mataifa mengine, milango ya uwekezaji na urasimu katika biashara na anadhamira ya kweli hivyo lazima tushirikiane nae kikamilifu kufikia malengo chama mkasimamie hayo” amesema.
Ameongeza kuwa “mkatatue kero za wananchi, Rais anaumia anapopokea kero ambayo ingeweza kutatuliwa ngazi za chini lakini mpaka inafika juu wakati ingeweza kutatuliwa ngazi za chini” amesema.
Amesema chama katika ngazi yake wakatatue changamoto ya upatikanaji mgumu wa dawa, wakatatue tatizo la miondombinu kuhakikisha TANROADS na TARURA wanatimiza majukumu yao, pia wakaondoe kero za mama lishe na baba lishe na kero zinazoyakabili makundi ya vijana na wazee.
Aidha ameagiza chama kwenda kusimamia kamati za ulinzi na usalama katika ngazi zote kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na kufanya shughuli zao bila kusumbuliwa huku wakifuata sheria za nchi.
Nae Waziri Mkuu msitaafu Mhe. Mizengo Pinda amepongeza kwa viongozi hao kufika katika ofisi kwa lengo la kujitambulisha huku akitaka kushirikiana kwa pamoja katika mapambano ya kuhakikisha wanasukuma gurudumu mbele za maendeleo hasa katika nyanja za kilimo.
Awali mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Godwin Mkanwa amesema mkoa wa Dodoma uko swari katika ngazi zote na kuahidi kutekeleza maagizo yote na kutoa ushirikiano kwa viongozi hao katika kukiendesha chama hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amewataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kwenda kusimamia agenda ya elimu na kuhakikisha katika maeneo yao wanafunzi waliopo katika madarasa ya mitihani wanapunguziwa kazi nyumbani ili kuelekeza nguvu katika kusoma ili kupandisha kiwango cha ufaulu kwa mkoa wa Dodoma.