……………………………………………………………………..
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Kufuatia elimu ya uchumi inayoendelea kutolewa kwa wananchi wa kata mbalimbali wilayani Ludewa mkoani Njombe wakazi wa kata ya Milo wilayani humo wamepewa amri ya kupanda miti ya matunda ya parachichi isiyopungua miti kumi kwa kila kaya ili kuweza kukuza uchumi kwa kupitia zao hilo la kimkakati ambalo limeonekana kuwa na soko ndani na nje ya nchi.
Amri hiyo imetolewa na diwani wa kata hiyo Robert Njavike wakati wa mkutano wa kampeni ya kukuza uchumi inayoendeshwa na ofisi ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kupitia muwezeshaji wake Lucia Mwaipopo kutoka mkoani 0Dodoma.
Njavike amesema ni lazima wananchi wote wa kata yake wapande miti hiyo ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwao katika kukuza uchumi hivyo mwananchi yeyeto atakayekaidi utekelezaji wa agizo hilo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ameongeza kuwa katika kufanikisha hilo atawagawia wananchi miche ya miti hiyo ili waanze kupanda sambamba na kufuatilia maendeleo ya miche hiyo ili kuona kama inapatiwa huduma stahiki.
“Ni lazima wananchi wangu mchangamkie fursa ya kilimo hiki kwani hali ya hewa ya kata yetu ni rafiki kwa zao hili, mimi nitahakikisha suala hili linafanikiwa kikamilifu maana hii ni njia mojawapo ya kukuza uchumi”, Alisema Njavike.
Aidha kwa upande wa wananchi waliohudhulia mkutano huo walionekana kukubaliana na kumuunga mkono diwani huyo kwa madai kuwa mkakati huo utawasaidia kuondokana na umasikini.
Hongera Jacob ni mmoja wa wananchi wa kata hiyo ambaye alihudhulia mkutano huo amesema kuwa binafsi ameturahishwa na kauli hiyo ya diwani wao kwani yeye ni mwanachama wa kikundi cha Uinjilisti ambacho tayari walishaanza uzalishaji wa zao hilo.
Amesema kwa sasa kikundi chao kina hekari nne la zao hilo na wameshaanza kuona faida yake kwani kikundi hicho kinamiliki kiwanda cha kusindika juisi za matunda mbalimbali ikiwemo parachichi.
Sanjali na hilo pia amemshukuru mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga kwa kuwaletea mtaalamu wa uchumi kwa ajili ya kuwapatia elimu ya kukuza uchumi ambayo itawasaidia kufanya shughuli za kiuchumi kulingana na soko la dunia.
Kampeni hiyo ya uchumi tayari imeshawafikia wananchi wa kata 15 kati ya 26 zilizopo wilani humo ambapo zoezi hilo litakuwepo kwa kipindi cha miaka miwili.
Hata hivyo kwa upande wa katibu wa mbunge wa jimbo hilo Alphonce Mwapinga amesema ofisi ya mbunge imeamua kuwaletea mtaalamu wananchi ili kuwawezesha kutumia fursa mbalimbali zilizopo hasa za kilimo ambapo ardhi ya Ludewa imebarikiwa kustawi mazao mengi zaidi.
Amesema wananchi wanapaswa kujikita katika kilimo cha kimkakati kwa mazao kama parachichi, kahawa, chai, korosho na mengineyo ambapo vitawasaidia wakulima kupata ujuzi na kulima kilimo cha kisasa na chenye tija.
Sambamba na kilimo pia amesema ofisi hiyo inawaelimisha wananchi kufuga mifugo ya aina mbalimbali kama kuku, ng’ombe, nguruwe, samaki na mifugo mingineyo kwa njia ya kisasa ili kuhakikisha ufugaji unawaletea faida.