***************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa mstaafu mhandisi Evarist Ndikilo amemkabidhi taarifa ya mkoa na ofisi ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,Aboubakar Kunenge, huku akimtaka apokee kilio cha wananchi wa Mailmoja ambao hawajui hatima yao hadi sasa ya ubomoaji barabara mita 120 kwa ajili ya upanuzi wa barabara.
Alimuomba kuliangalia na kusimamia suala sugu la kuvunja eneo la upande wa kushoto mita 120 na kulia 120 ambalo yeye alilizuia kwa kipindi chote cha miaka saba ,kwani mji wa Kibaha ndio sura na kioo cha mkoa.
Ndikilo ,alisema ,suala hilo ni gumu ,limalize ili watu wabaki na amani na waweze kujiendeleza kiuchumi,kwakuwa sasa wananchi hao hawaijui kesho yao.
“Nilipambana kuzuia ubomoaji huu ,kwa maslahi ya jamii ,lingeleta maumivu makubwa kwa wananchi ,naomba ulisimamie hili na ulimalize ,Nilishakaa na mawaziri husika lakini nenda kalisimamie na wewe ” alisisitiza Ndikilo.
Alielezea kwamba ,amefanya kazi kwa miaka 34 akiwa serikali ,na anashukuru na serikali kumpa nafasi mbalimbali kuongoza.
Ndikilo alielezea kuwa ,Rais Samia amefanya uteuzi sahihi kwa kumchagua Kunenge kupokea kijiti kwani ni mchapakazi na kiongozi muwajibikaji.
Aliwapongeza wakuu wa wilaya kwa ushirikiano nae na kusaidiana kwa maslahi ya mkoa na kuzipongeza halmashauri kwa kupata hati safi katika kipindi chake .
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Kunenge alisema ameingia katika utumishi wa kisiasa miezi kumi sasa.
Alisema kwa umoja na ushirikiano watafanikiwa na ameomba watumishi na wataalamu kuchapakazi .
Kunenge alizitaka halmashauri chini ya watendaji wake wakaondoe kero na kutoa huduma kwa wananchi .
Awali katibu tawala wa mkoa wa Pwani,Delphine Magere alisema Ndikilo aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo mwaka 2014 ,June hadi kufikia kustaafu mei 2021.
Alieleza,mkuu wa mkoa mstaafu akiwa mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ,amestaafu akiwa mkuu wa mkoa huo kwa miaka saba.
“Mkuu huyo ameacha alama kubwa katika sekta zote kubwa zaidi kuinua sekta ya viwanda na uwekezaji,ni mzazi ,mwalimu wangu ,mchapakazi ,anaebeba changamoto na kujua kuishi na watendaji wake ,” alifafanua.
Nae katibu wa CCM Pwani,Elias Mpanda alieleza Ndikilo amekiacha chama kikiwa na ushirikiano na mahusiano mzuri na Serikali .
Alisema ,anamjua Kunenge hivyo anaamini ataendeleza mahusiano hayo na kuiimarisha chama na serikali .