Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza na ugeni wa wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank (AfDB) kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Farkwa.
Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Maji wakimsikiliza Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja na Wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Dkt. George Lugomela akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya watendaji wa Wizara na Watalaam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiwa katika picha ya pamoja na ugeni wa wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank (AfDB) na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Maji.
………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amekutana na wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank (AfDB) na kufanya nao mazungumzo kuhusiana na ujenzi wa bwawa la Farkwa.
Mhandisi Sanga amefanya kikao na wataalam hao katika ofisi za Wizara katika mji wa serikali Jijini Dodoma.
Wataalam hao wapo katika ziara ya maandalizi ya awali ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Farkwa ambapo Mhandisi Sanga amesema serikali imejiandaa kwa mradi huo ikiwamo kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo wanatakiwa kuhama na kupisha ujenzi.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeonesha nia ya ya kushiriki katika kazi ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa.
Akizungumza kwa niaba ya (AfDB) Bwana Benson Nkhoma amesema awali katika kufanya maaandalizi ya utekelezaji wa mradi huu walifanya vikao viwili mapema mwaka huu kwa njia ya kieletroniki.
Amesema katika vikao hivyo walikubaliana kuwe na ziara ya maandalizi ya utekelezaji wa program ili kukusanya taarifa na takwimu za msingi.
Watalaam hao kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika wamepata fursa pia ya kufanya kikao na Maafisa wa Wizara ya Fedha na Maafisa wa Ofisi ya Makamu wa Rais kujadili kwa upana utekelezaji wa mradi wa bwawa la Farkwa linalotarajiwa kuongeza huduma ya maji katika Jiji la Dodoma.