Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Babati.
********************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MAHAKAMA ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imemuhukumu kifungo cha miaka miwili kwenda jela aliyekuwa Ofisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ezekiel Mayumba, kwa kosa la kughushi nyaraka, kumdanganya mwajiri na ubadhirifu wa fedha za chanjo shilingi milioni 6.
Akizungumza Mjini Babati na waandishi wa habari, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza amesema Mayumba amehukumiwa na hakimu mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Owiso.
Makungu amesema baada ya kumaliza kutumikia kifungo hicho cha miaka miwili, Mayumba anatakiwa kurejesha fedha hizo shilingi milioni 6.
Amesema mshtakiwa huyo Mayumba ametiwa hatiani kwa makosa ya kumdanganya mwajiri, kughushi nyaraka na ubadhirifu wa shilingi milioni 6.
Makungu amesema awali, mawakili wa TAKUKURU, Martin Makani na Evaline Onditi walimfikisha Mayumba mahakamani na kudhibitisha kuwa mashtakiwa huyo alitenda makosa hayo.
Amesema mawakili hao wamedhibitisha kuwa Mayumba alipewa jukumu la kusimamia shughuli ya chanjo ya Rubela na Surua, Wilayani Simanjiro, mwaka 2014 na alipewa shilingi milioni 75.
Amesema kwenye kufanya marejesho namna fedha zilivyotumika, alitumia stakabadhi za kughushi kuwa alilipia washiriki 411 kwa shilingi milioni 6.
Amesema ilionyesha fedha hizo zimetumika kwa ajili ya viburudisho, maji na chakula za washiriki hao kwenye mgahawa wa Orkesumet unaomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Arusha, Maelezo ambayo upande wa mashtaka umedhibitisha kuwa siyo kweli.
Amesema Mahakama iliridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka usiotia shaka kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili na kulipa shilingi milioni 6 baada ya kumaliza kutumikia kifungo.
“Tunaendelea kutoa wito kwa watumishi wa umma kujiepusha na ubadhirifu wa mali ya umma kwa kuridhika na ujira wa haki wanaolipwa na wajiri wao,” amesema Makungu.