Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel.akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha baada ya kutunukiwa Tuzo ya Heshima na Kampuni ya Phide Intertermet and Tours yenye makao yake makuu jijini Arusha inayojishughulisha na masuala ya utalii hapa nchini.
Hii ni moja kati ya Tuzo nane alizowahi kutunukiwa.
Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Phide Intertermet and Tours yenye makao yake makuu jijini Arusha inayojishughulisha na masuala ya utalii hapa nchini imemtunuku Tuzo ya Heshima Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel kutokana na mchango wake mbalimbali katika jamii.
Akizungumza kwa furaha baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo Joel aliishukuru kampuni hiyo kwa kutambua mchango wake anaoutoa kwa jamii.
” Naishukuru kampuni hii kwa kunitunuku Tuzo hii ya heshima kutokana na mchango wangu katika jamii kupitia TAMUFO na vyama vingine ambavyo ni mwanzilishi ambavyo niliviongoza.” alisema Joel.
Alisema Tuzo hiyo kati ya nane ambazo amewahi kutunukiwa
imempa nguvu na ari ya kuendelea kutumikia jamii katika nyanja mbalimbali pindi atakapokuwa anapata nafasi ya kufanya hivyo.
Joel alisema licha ya kutunukiwa Tuzo hiyo siyo yake peke yake bali ni ya wote alioshirikiana nao kwa njia moja au nyingine katika kazi hizo alizozifanya na kuonekana katika jamii na hatimaye kutunukiwa tuzo hiyo ya heshima.
” Tuzo hii ni yetu sote maana bila ya ushirikiano wenu nisingeweza kuipata kwani imenipa hamasa na kunitia moyo sana.” alisema Joel.
Katibu Mkuu huyo wa TAMUFO alitumia nafasi hiyo kuishukuru Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Kampuni ya Phide Intertermet and Tours Wanahabari kupitia vyombo vyao mbalimbali pamoja na wadau wote wa maendeleo kwa ushirikiano wao wa mara kwa mara wanaompa wakati akitekeleza majukumu yake.
Mlezi wa TAMUFO, Frank Richard alimpongeza Joel kwa kutunukiwa Tuzo hiyo akamtaka kutolewa sifa badala yake aendeleze moto wa kufanya kazi na kuwa mbunifu zaidi jambo litakalo panua wigo mkubwa wa kuwatumikia wanamuziki na jamii kwa ujumla.