Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo akizungumza na wandishi wa habari leo Mei 20,2021 jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa katibu Mkuu wa Chama hicho.
Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu Bara, Christina Mndeme wakati mara baada ya kumaliza kuongea na wandishi wa habari leo Mei 20,2021 jijini Dodoma.
Katibu wa NEC,Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na wandishi wa habari jijini Dodoma leo.
…………………………………………………..
Na Ezekiel Mtonyole Dodoma.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Daniel Chongolo ametaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwa wote walioshiriki katika uzembe na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma ya umeme baada ya mfumo wa luku kushindwa kufanya kazi siku ya jana.
Katibu mkuu Chongolo ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa maelekezo maalumu kwa Wizara tatu, ambapo amesema lazima uchunguzi ufanyike na atakayebainika kusababisha uzembe huo serikali ichukue hatua kali.
“Nionye wale wenye nia ovu na Nchi yetu ambao walitaka kutuweka gizani uchunguzi hufanyike tena wa kina, niipongeze Serikali kwa hatua za awali walizochukua katika kuhakikisha wananchi wanaepukana na changamoto ya manunuzi ya umeme” amesema.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Chongolo ametoa maagizo kwa Wizara tatu vipaumbele vya kutekeleza ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Nishati.
Chongolo ameiagiza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kuhakikisha inamaliza kwa wakati miradi yote ya Nishati ambayo imeanza kutekelezwa ukiwemo mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere uliopo Rufiji mkoani Pwani.
Katibu Mkuu Chongolo amesema kumalizika kwa mradi huo kutaongeza megawati za umeme zipatazo 2115 na kusaidia kuwa na umeme mwingi jambo ambalo litakuza uchumi wa Nchi kupitia viwanda.
” Lakini pia tunaiagiza Serikali kumalizia kuweka umeme vijiji ambavyo vimebaki kwani Ni vichache sana, lengo la Chama chetu ni kuona Nchi nzima inawaka umeme ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa Taifa letu,” Amesema Chongolo.
Kuhusu Wizara ya Ardhi, Chongolo ameielekeza Wizara hiyo kuongeza kasi yake ya utoaji hati kwa wananchi katika kumiliki ardhi hatua ambayo itasaidia kuwafanya wananchi kuwa na usalama na ardhi yao.
” Tunaelekeza wizara kuongeza kasi kwenye suala la umiliki wa maeneo, CCM kupitia ilani yake ibara ya 74 imeielekeza Serikali kuongeza kasi ya utoaji hati na sisi kama Chama tutalisimamia hili kwa weledi na tunataka kuona Wizara kupitia bajeti yake watueleze wamejipanga kiasi gani kuondoa adha hiyo ya kupoteza ardhi zao kwa kukosa hati.
Kwenye usaminishaji na fidia CCM inaielekeza Serikali kuwalipa wananchi stahiki zao kwa wale wote waliotwaliwa maeneo yao kisheria, na niwaagize viongozi wetu kuanzia ngazi ya Mitaa na Vijiji hadi Wizarani kutatua changamoto za ardhi,”amesema Chongolo.
Kwenye sekta ya Kilimo, Katibu Mkuu Chongolo ameielekeza Wizara ya Kilimo kukamilisha ujenzi wa skimu katika wilaya ya Songea na Rungwe huku akiitaka Serikali pia kuongeza tija na faida katika uzalishaji wa mazao.
” Kutokana na kuwa na changamoto ya mbegu Chama kinaielekeza Serikali kuongeza bajeti ya utafiti wa mbegu ili kuwahakikishia wakulima ubora wa mbegu wanazonunua,” amesema Chongolo.
Aidha ameiagiza kufunguliwa kwa mashamba ya kimkakati katika mazao ya mafuta hasa mazao ya alizeti, chikichi na kalanga ili kupunguza uhaba wa mafuta unaopelekea kama nchi kuagiza nje.
Pia ametaka kujengwa kwa maghala maeneo ya mipaka ya nchi ili kusisimua biashara na kuwa na mazao salama, Vilevile ametaka kujengwa kwa maghala katika maeneo yote yanayozalisha mazao kwa wingi hapa nchini.
Pia ametoa onyo kali kwa watendaji na watumishi wa umma ambao wamekuwa wakilumbana katika utendaji kazi wao na kupelekea migogoro na kushindwa kuwatumikia wananchi