Maafisa wa Wakala wa Vipimo (WMA) wakihakiki mizani katika hospitali ya Vijibweni Kigamboni leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea katika hospitali hiyo kama maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani.
Fundi wa mizani zilizoharibika mwenye leseni ya WMA akiendelea na ufundi wa mizani katika hospitali ya Vijibweni wilayani Kigamboni leo Jijini Dar es Salaam.
PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
*************************
NA EMMANUEL MBATILO,DAR ES SALAAM
Wakala wa Vipimo(WMA) wameendelea kutembelea katika vituo vya afya kwa ajili ya kuhakiki mizani zinazotumika katika vipimo ikiwa na madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “VIPIMO KATIKA SEKTA YA AFYA”.
Akizungumza mara baada ya kutembelea katika hospitali ya Vijibweni Kigamboni Kaimu Meneja WMA mkoa wa Temeke Bw.Krishna Mahamba amesema katika uhakiki wao wa mizani wamekuta ipo vizuri na kuziruhusu ziweze kutumika na ambazo hazipo vizuriwanazifanyia utaratibu wa maboresho ya matengenezo kwa mafundi ambao wana leseni ya kutengeneza mashine hizo.
Aidha Bw.Mahamba amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa kuhakiki mizani kwa maana kuna muepusha mgonjwa kupata madhara ya afya anapotumia dozi.
“Kile kipimo ambacho kinampima mtoto kama hakitoi matokeo sahihi tunaweza kusema mtoto amezaliwa na kilo 1 kumbe ana kilo 5 au mtoto amezaliwa na kilo 6 kumbe ana kilo 2 kwahiyo hata zile huduma za kitabibu hazitaendana sawa na huduma inayostahili”. Amesema Bw.Mahamba.
Amesema uhakiki wa vipimo ni endelevu na vinahakikiwa vipimo vyote Tanzania bara kwa kufuata sheria za vipimo ambazo ambapo kila kipimo angalau kihakikiwe mara moja ndani kipindi cha miezi 12 au pale mtumiaji ama mnunuzi atakapokuwa na wasiwasi na kile anavhokipata kwenye kipimo lazima kirudiwe kuhakiki kipimo ili kuhakikisha kwamba kile kinachopimwa ni halisia kulingana na usahihi wa kile kipimo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Vijibweni Bw.Thomas Bwire amesema wamekuwa wakifanya zoezi la kuhakiki vipimo mara kwa mara kwasababu vikiwa sahihi na huduma pia zinaweza kuwa sahihi.
“Kuna dawa zinatakiwa kutolewa kulingana na uzito wa mgonjwa kwahiyo kama hauna kipimo sahihi unaweza kumpa mgonjwa kiwango cha dawa kisichoendana na uzito wake hivyo unaweza kumzidishia dawa ama kumpunguzia dawa na matokeo yake kunaweza kumfanya mgonjwa kutopata matibabu sahihi na asiendelee kupata uponyaji uliokubalika”. Amesema Bw.Bwire.