Mtaalam wa maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jesca Mlay akimtoa damu mchezaji wa timu ya taifa ya ufukweni (Beach Soka) Shabani Kodo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya mwili wakati wachezaji 16 wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Senegal tarehe 23 hadi 30 Mei mwaka huu.
Radiografa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Shaniath Mzirai akimpima X-ray ya kifua kuchunguza moyo na mapafu mchezaji wa timu ya taifa ya ufukweni (Beach Soka) Kashiru Salum kwa kutumia mashine ya X-ray wakati wachezaji 16 wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Senegal tarehe 23 hadi 30 Mei mwaka huu.
Fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Gerson Mpondo akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) mchezaji wa timu ya taifa ya ufukweni (Beach Soka) Stanley Mkomola wakati wachezaji 16 wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Senegal tarehe 23 hadi 30 Mei mwaka huu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Engelasia Kifai akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) mchezaji wa timu ya taifa ya ufukweni (Beach Soka) Abdulkadir Ali wakati wachezaji 16 wa timu hiyo walipofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Senegal tarehe 23 hadi 30 Mei mwaka huu.
Picha na: JKCI
*********************************
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
19/05/2021 Wachezaji 16 wa timu ya Taifa ya Ufukweni (Beach Soka) wamefanyiwa uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linavyoelekeza kabla ya kuanza kwa mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ni lazima wachezaji wanaoshiriki mashinadano hayo wapimwe afya zao.
Upimaji huo licha ya kuangalia afya ya moyo pia uliangalia afya ya mwili kwa ujumla umefanyika leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Vipimo walivyofanyiwa wachezaji hao ni vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG), kipimo cha X-ray ya kifua kinachochunguza moyo na mapafu na vipimo mbalimbali vya damu.
Akizungumza wakati wa upimaji huo Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala alisema upimaji kwa wachezaji hao umeenda vizuri na kuleta majibu chanya katika kila kipomo walichofanyiwa.
Dkt. Mayala alisema timu mbalimbali ambazo zinashiriki mashindano ya kimataifa zimekuwa zikifika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo lakini wachezaji hao kwa mara ya kwanza wamefanyiwa uchunguzi wa kipimo cha X-Ray ya kuchunguza mapafu na moyo tofauti na ilivyokuwa kwa wachezaji wengine waliofanyiwa vipimo.
“Leo Taasisi yetu imepata fursa ya kuwafanyia uchunguzi wa afya ya moyo na mapafu wachezaji 16 wa Timu ya Taifa ya Ufukweni (Beach Soka) ambapo kila mchezaji alichunguzwa kwa kina na majibu ya vipimo vyao yameonesha wachezaji wote wapo sawa kiafya na hivyo kukidhi vigezo vya kushiriki michezo wanayotarajia kwenda kushiriki”
“Ninaamini yakuwa matokeo chanya ya vipimo tulivyowafanyia yanatokana na umahiri wao katika mazoezi wanayoyafanya kila siku. Nitoe rai kwa wananchi wengine ambao sio wanamichezo kuwa na tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara hii itawawezesha kujenga afya iliyo bora na kuepukana na maradhi yasiyo ya kuambukiza” alisema Dkt. Mayala.
Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Dkt. Norman Sabuni alisema uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa kwa wachezaji 16 wa timu ya Taifa ya Ufukweni (Beach Soka) unaambatana na safari ya kushiriki fainali za kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Soka la Ufukweni yatakayofanyika nchini Senegal mwishoni mwa mwezi Mei.
“Tumekuwa tukiwapima afya wachezaji wa timu zetu za taifa mara kwa mara bila ya kusubiria michuano mbalimbali wanayoshiriki, hii imekuwa ikisaidia kuwaweka sawa wachezaji na kuwapatia tiba mapema pale wanapokutwa na changamoto yoyote ya afya kabla ya kuanza kwa michuano”, alisema Dkt. Sabuni.
Naye kapteni wa Timu ya Taifa ya Ufukweni (Beach Soka) Rolland Msonjo alisema amefurahishwa na majibu ya vipimo vya wachezaji wa timu yake kuwa mazuri kwani kwa kuwa na afya bora ni mwanzo mzuri wa wachezaji hao kwenda kushindana na kurudi na ushindi.
Timu mbalimbali zimeshafanyiwa vipimo hivyo katika Taasisi hiyo zikiwemo Taifa Stars wakati inashiriki mashindano ya mataifa ya Afrika na wachezaji wanaocheza ligi za ndani Barani Afrika (CHAN),timu ya Simba, timu ya taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes na timu ya taifa chini ya miaka 17 Serengeti Boys.