MBUNGE wa Jimbo la Mkinga mkoani Tanga (CCM) Dunstan Kitandula ameonyesha kusikitishwa na kitendo cha kusahaulika kwa barabara ya Mabokweni – Maramba, Mtoni Bombo hadi Korogwe kwenye makutano ya Umba mpaka Same wilayani Kilimanjaro ambayo amekuwa akiizungumzia kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo bungeni.
Amesema barabara hiyo ilikwisha kuahidiwa na Marais watatu ambao ni Hayati Benjamini Mkapa,Jakaya Kikwete na hayati Dkt John Magufuli lakini kwa kushangaza haipo hata kwenye upembuzi yakinifu jambo ambalo linamsikitisha kutokana na namna alivyoipigania kila wakati bila mafanikio.
Kitandula aliyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia hoja wakati wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambapo alianza kwa kukishukuru Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya kwanza kutambua umuhimu wa Barabara ya Maramba –Mabokweni Mtoni Bombo kuelekea Korogwe na makutano ya Umba mpaka Same na kuiingiza kwenye ilani ya CCM ya Uchaguzi.
Mbunge Kitandula alisema lakini licha ya kuingia kwenye ilani kwa masikitiko makubwa bajeti hiyo imeisahau barabara hiyo ambayo aliizungumzia miaka 10 mfululizo huku wakipewa ahaidi kwa vipindi tofauti kwamba itajengwa kwa kupitia MCC kipindi fulani mpango ambao uliyeyuka; na kwa wakati mwengine aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akahaidi kwamba barabara hiyo itaingizwa kwenye mpango wa usanifu lakini mpaka leo haitajatokea.
“Lakini pia Barabara hii ilihaidiwa na Marais Watatu Benjamini Mkapa,Jakaya Kikwete na John Magufuli lakini cha kushangaza haipo hata kwenye upembuzi yakinifu”
“Barabara hii kwa nyakati tofauti imezungumziwa vilevile na Shehe Mkuu wa Tanzania Mufti Shehe Abubakari Zuberi ambaye alipewa ahaidi na Rais Hayati John Magufuli pale Korogwe na haijatokea…halikadhalika Askofu Mkuu wa Angalikana aliizungumzia barabara hii naye akaahidiwa itajengwa na haijajengwa. Akionesha msisitizo Kitandula akahoji kama mmepuuza maneno ya Kitandula hata hawa viongozi nao mnayapuuza, hivi muambiwe na nani ili muelewe”Alihoji Mbunge Kitandula.
Mbunge Kitandula alisema kwamba watu wa Mkinga waanasikitika sana na jambo hilo huku aakieleza kwamba anataka kuweka rekodi sawa kwamba kuna maneno yanasemwa kuwa watu wa Kaskazini wamependelewa jamani Tanga hatuna barabara,Mkinga hatuna barabara huku Mkinga wana kilomita zisizozidi kilomita 25 za lami ambazo zinakwenda mpakani Horohoro na hazikwenda kwenye maeneo ya uzalishaji.
“Hebu tutendeeni haki twendeni mkatusaidie kujenga barabara ya kutoka Mabokweni ,Maramba,Mtoni Bombo,Mashewa kwenda Korogwe lakini tuunganishe na barabaa ya kwenda Umba makutano mpaka Same”Alisema
Hata hivyo alisema kwamba hivi sasa kwa upande wa wilaya ya Same Mkoani Kilimanajaro upembezi yakinfu wa barabara hiyo umekamilika akahoji kwanini kunakuwa kigugumizi kwa upande wa Tanga, hivyo wanamuomba Waziri awaeleze kuhusu barabara hiyo
Akiendelea kuchangia alisema kuna barabara imeanza kujengwa kwenda makao makuu ya wilaya ya Mkinga lakini cha kushangaza na kichekesho wanajenga mita 200,mita 150 kwenye barabara yenye kilomita 48 akahoji tunapojenga hivi tutamaliza lini; hivyo ninaiomba serikali ifikirie mambo hayo”Alisema Mbunge Kitandula.