……………………………………………………………………..
MBUNGE wa Nanyamba (CCM) Mhe.Abdallah Chikota, ameiomba Serikali kuweka vivutio maalum vya kuvutia wawekezaji kwenye viwanda vya kubangua korosho.
Akiuliza swali hilo leo Mei 19,2021 bungeni jijini Dodoma ambalo Mhe. Chikota amehoji kuwa Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka vivutio maalum ili kuvutia Wawekezaji kwenye viwanda vya kubangua korosho.
“Viwanda vimeajiri vijana na kinamama wengi na vinafanya kazi chini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosekanaji wa malighafi sababu hawapati korosho mnadani,” amesema Mhe.Chikota
Alihoji serikali inatoa kauli gani kwa wawekezaji waliofungua viwanda nchini na wanaotarajia kuja kuwekeza.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji,Mhe. William Ole Nasha,amesema kuwa Serikali imeahidi kuboresha mfumo wa soko la awali kwa wabanguaji wa ndani wa zao hilo ili uvutie na wakulima wasione kama wanatumia mfumo wa kangomba.
Hata hivyo Mhe.Ole Nasha amemhakikisha Mhe.Chikota kuwa kwa sababu ndio mfumo huo umeanza utaboreshwa zaidi ili uweze kuvutia wakulima.
Amesema kuwa Serikali inafikiria kuona namna bora ya kuhakikisha korosho inapatikana kwa wingi ili ajira zipatikane kwa vijana.
Mhe.Ole Nasha amesema kuwa Serikali inatekeleza mpango wa uhamasishaji wa kilimo cha korosho katika mikoa yote inayostawisha kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, huduma za ugani na pembejeo ili kuimarisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda nchini.
“Hadi sasa takribani mikoa 20 inazalisha zao hilo kwa viwango tofauti na msimu wa mwaka 2020/21 uzalishaji ulikuwa tani 200,010 na kuipatia nchi kiasi cha sh. Bilioni 477,”amesema Mhe.Ole Nasha
Ameeleza kuwa ili kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho, Serikali imeweka vivutio mbalimbali ikiwemo vivutio visivyo vya kikodi kama vile kuweka mfumo wa soko la awali kwa wabanguaji wa ndani kuanzia mwaka, 2020.
“Lengo ni kuwawezesha kununua korosho bila kushindana na wanunuzi wanaosafirisha korosho ghafi kwenda masoko ya nje ya nchi na kuwahakikishia malighafi kwa bei nafuu,”amesema.
Pia ameongeza kuwa katika mnada huo jumla ya tani 2,021.7 zimenunuliwa na viwanda tisa vilivyoshiriki soko hilo la awali.
Mhe.Ole Nasha amesema kuwa serikali imeweka pia vivutio vya kikodi kwa Viwanda vya kubangua korosho kupitia Sheria ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje Sura 373 ikiwemo msamaha wa Kodi ya Makampuni (Corporate tax) kwa miaka 10.
“Msamaha wa asilimia 100 wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za mtaji, Msamaha wa asilimia mia moja wa Kodi ya Zuio kwa Riba ya mikopo kutoka nje, pango na gawio na Msamaha wa asilimia 100 wa Kodi ya Ushuru wa Forodha kwa Mitambo na Vifaa,”.
Hata hivyo amesema kuwa kupitia utaratibu huo, jumla ya viwanda tano vimesajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZ).
Amefafanua kuwa serikali itaendelea kubuni na kuweka vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuvutia zaidi uwekezaji ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwenye Halmashauri zinazolima korosho hapa nchini.
”Ambapo maeneo hayo yatakuwa na huduma muhimu kama vile umeme, maji na barabara na kupitia kodi mbalimbali zinazotozwa katika mitambo, vipuri na vifungashio”amesema