Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu TBS wakati wa semina ya kujenga uelewa na uwasilishaji taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma Mei 18,2021.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Yusuph Ngenya akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TBS kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma Mei 18,2021.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe akijibu hoja mbalimbali zinazohusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati wa semina ya kujenga uelewa kuhusu TBS kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma Mei 18,2021.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Askofu Josephat Gwajima akichangia hoja zinazohusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati wa semina ya kujenga uelewa kuhusu TBS kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma Mei 18,2021.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akijibu hoja mbalimbali zinazohusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati wa semina ya kujenga uelewa kuhusu TBS kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma Mei 18,2021.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akiongoza semina ya kujenga uelewa na uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma, Mei 18,2021.
Meneja Udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. Gervas Mwanjabala akijibu maswali na hoja zilizoulizwa na wanakamati wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakati wa semina ya kujenga uelewa kuhusu TBS ,Bungeni Dodoma Mei 18,2021
.
Picha zote na Eliud Rwechungura
……………………………………………………………………………
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na utoaji wa elimu kwa wajasiliamali ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazoendana na kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda na kuwezesha biashara shindani nchini.
Hayo yalisemwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile(Mb) wakati wa semina iliyolenga kuwajengea uelewa wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo iliyofanyika leo tarehe Mei 18,2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara. Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb) wakati akijibu hoja, maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira alisema Serikali imeendelea kuiwezesha TBS kuboresha utoaji wa huduma zake.
Nao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha huduma na bidhaa zinazotolewa na TBS na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu huduma hizo.
Maoni hayo yalijumuisha uboreshaji wa huduma ya ukaguzi wa magari yanayoingia nchini, udhibiti wa ubora wa chakula hususani nyama na nafaka, upimaji wa bidhaa zenye GMO zinazoingia nchini, vinasaba vya mafuta na utoaji wa nembo za ubora wa bidhaa mikoani ili kusogeza huduma hizo kwa wananchi katika maeneo husika.
Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt Yusuph Ngenya alisema TBS imepitia na kupunguza mchakato wa muda unaotumika kuandaa viwango ili kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda na kuwezesha biashara nchini.
Naye Meneja Udhibiti Ubora, Bw. Gervas Mwanjabala wakati akiwasilisha taarifa kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, alisema TBS ina maabara tisa (9) zilizopo katika ofisi za Makao Makuu ya Shirika, Ubungo Dar es Salaam. Kati ya maabara tisa (9), maabara saba (7) zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya umahiri au ithibati (Accreditation), maabara hizo ni pamoja na Maabara ya Ugezi, Maabara ya Kemia ya Chakula, Maabara ya Maikrobaiolojia; Maabara ya Kemikali; Maabara ya Uhandisi Ujenzi; Maabara ya Uhandisi Mitambo; na Maabara ya Uhandisi Umeme
Aidha, Meneja huyo alisema kuwa TBS inaendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia TEHAMA ili ziendane na wakati na kukidhi mahitaji ya wateja na inampango wa muda mfupi wa kuingia makubaliano na Maabara ya Taifa ya Udhibiti Ubora wa Samaki (NFQCL), Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) na Maabara ya Maji Mwanza ili kukidhi ongezeko la uhitaji wa huduma za uchunguzi wa usalama na ubora wa bidhaa hasa za chakula
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianzishwa kwa juhudi za Serikali kama sehemu ya jitihada ya kuimarisha Miundombinu ya sekta ya Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa. TBS ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 3 ya Mwaka 1975 na kuanza rasmi tarehe 16 Aprili 1976 ambapo ilipewa jukumu la kuratibu uandaaji wa viwango na kusimamia utekelezaji wake.
Aidha, TBS iliongezewa uwezo mkubwa wa kusimamia shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora wa bidhaa kupitia Sheria ya Viwango Na.2 ya Mwaka 2009. Kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Fedha Na.8 ya Mwaka 2019, Shirika liliongezewa majukumu mapya ya kusimamia usalama na ubora wa bidhaa za chakula na vipodozi