……………………………………………………………………….
Na Adeladius Makwega,Babati–Manyara
Serikali imesema kuwa sasa ni wakati sahihi wa kuanza kupeleka fedha za michezo ngazi za chini ambazo zitatumika kuongeza kasi ya maendeleo ya michezo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi Pauline Gegul wakati wa ufunguzi wa Kongomano la Wadau wa Michezo Mkoani Manyara lililoratibiwa na Wilaya ya Babati.
“Kwa sasa fedha ya maendeleo ya michezo inayopelekwa katika ngazi ya chini na shuleni ni ile ya uendeshaji wa shule kwa shule zetu za msingi na sekondari tu na inaitumika kwa ajili ya manunuzi ya vifaaa vya michezo” amesema Mheshimiwa Gekul.
Ameongeza kuwa Waziri mwenye dhamana ya Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Mheshimiwa Innocent Bashungwa amekutana na Waziri wa Mipango na Fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa lengo la kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambao kwa sasa bado suala hilo linafanyiwa kazi kwa kina juu ya vyanzo vyake vya fedha.
“Jukumu lenu nyinyi kama wadau wa michezo mara tu mfuko huu ukianzishwa basi kila mmoja wetu achangie ili kuweza kufanikisha lengo hilo la kukuza michezo kwa taifa letu”alihimiza Mheshimiwa Gekul.
Aidha, Mheshimwa Gekul amewapongeza Madiwani na Wabunge nchini kwa kudhamini na kufadhili michezo kutoka ngazi ya vijiji, kata na wilaya jambo ambalo amedai kuwa limefanya baadhi ya vijana nchini kufanya vizuri kitaifa na Kimataifa.
Akizungumza katika kongamano hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Alpha Matipula amesema kuwa hali ya michezo Wilayani Babati ni nzuri kwani kwa kiasi kikubwa wadau wote wa michezo wanashirikiana vizuri.
“Changamoto zipo, lakini nina imani Serikali na wadau wote tutazitatua kero hizo lakini ni wajibu wa wadau wa michezo kuepuka migogoro ndani ya vilabu vya michezo” aliongeza Katibu Tawala huyo ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ngazi ya wilaya.
Wakizungumza katika kongamano hilo washiriki wameipongeza Serikali kwa kuwapa ushirikiano katika michezo na pia kwa kushiriki katika kongamano hilo. Wamesema vikundi vya Sanaa kama vile ngoma za asili ni vizuri kuheshimiwa kwa kulipwa kiasi kizuri cha fedha pale wanapofanya maonesho yao ili kuwasaidia kwani sanaa, michezo na utamaduni ni ajira.
Kwa upande wake Zulfa Mbaba ambaye ni mwalimu wa michezo katika shule ya msingi Hallu iliyopo Babati Vijijini akichangia mara baada ya kongamnao hilo kwisha amesema kuwa amejifunza mengi ndani ya kongamano hilo na amekutana na wadau wengi wa michezo ambao ilikuwa ngumu yeye kuwafikia na kuwafahamu lakini sasa atawatumia katika kuhamasisha michezo shuleni kwake.
Amebainisha kuwa watoto wanashiriki michezo shuleni kwa muda mrefu na michezo hiyo inaongeza ushindani pia katika masomo.
“Michezo inaibua ushindani na wivu wa maendeleo baina ya watoto shuleni nina imani mwanafunzi ambaye anafanya vizuri katika michezo anaweza kuhimizwa kufanya vizuri katika taaluma na yule anayefanya vizuri kitaaluma anaweza kuhimizwa kufanya vizuri kimichezo lakini kama vyote hivyo viwili vikifanyika vizuri.”
Kongamano hilo limewahusisha wakuu wa shule za msingi na sekondari, walimu wa michezo, viongozi wa vilabu vya michezo, wanamichezo bora wa zamani, maafisa michezo wa Wilaya na Mkoa huku lishamirishwa na ushiriki wa Mshindi wa Ulimbwende Wilaya ya Babati mwaka 2021 Bi Annet Japhert.