MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameiomba serikali kuongeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Singida- Kwamtoro-Kiberashi hadi Tanga ambayo ni ya kihistoria na ni muhimu kiulinzi na kiusalma kutokana na kupita sambamba na bomba la mafuta linalotoka Tanga kwenda Hoima.
Aidha ameishauri serikali kuongeza bidii katika utoaji wa tangazo la serikali GN ili kusaidia miradi itekelezwe kwa wakati.
Akichangia bajeti ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mei 17 bungeni,Mtaturu amesema barabara hiyo yenye kilomita 461 ni muhimu kiuchumi.
“Tumeangalia kwenye randama nimeona sasa imetengewa kilomita 20 badala ya 50 zilizotajwa mwanzoni,kutokana na bajeti hii ina maana itachukua muda mrefu kujengwa na kukamilika,niiombe serikali iongeze fedha ili kumaliza barabara hii kwa wakati maana imesubiri kwa muda mrefu,”amesema.
Amesema suala la GN limekuwa ni kikwazo kikubwa na kusababisha uwepo wa urasimu katika eneo hilo.
“Pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali yetu,niwaombe sana serikali waondoe urasimu ucheleweshaji wa GN,hizi fedha ambazo tunasema leo zimetoka haziwezi fanya kazi mpaka GN itoke,hili limekuwa ni kikwazo katika maeneo mengi,wakandarasi wanakuwa tayari lakini wanazuiliwa,muda mwingine mradi una miaka miwili au mitatu,ukiisha ule muda wa rot ya kwanza unakuta huwezi kuendelea mpaka GN itoke tena,”alisisitiza.
Amesema changamoto ya GN inaenda sambamba na utoaji wa fedha za miradi ambayo wamekuwa wakipitisha bajeti kila mwaka lakini fedha zimekuwa zinachelewa kutolewa na wakandarasi hawalipwi kwa wakati hivyo kuiomba serikali kuwalipa kwa wakati ili wawe na nguvu ya kutekeleza miradi wanayopatiwa.
Ombi lingine alilotoa Mtaturu ni serikali kuangalia upya maelekezo waliyotoa awali ya kuuruhusu Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD),kujenga viwanja vya ndege na badala yake kwa sasa iachiwe Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ifanye kazi hiyo.
“Huko nyuma viwanja vyetu vya ndege walikuwa wanajenga wenyewe mamlaka ya ndege kwa mujibu wa sheria na walikuwa wanasimamia piai,lakini baadae TANROAD walipewa jukumu hilo,sina tatizo na TANROAD ni wazuri sana,kwenye maeneo ya run ways wanajenga vizuri sana lakini kuna changamoto ya facilities nyingine katika viwanja vya ndege,
“Niiombe serikali sasa wafikirie upya,wawarudishie mamlaka ya viwanja vya ndege wajenge wenyewe viwanja vyao na ili wasimamie vizuri ni lazima wajenge wenyewe kwa kuangalia facilities inayotakiwa kwenye viwanja hivyo ikiwemo aiport tower ,lounge ya kusimamia kuchukulia abiria,”alisisitiza.
Aidha,amezungumzia barabara ya Mkiwa,Itigi mpaka Rungwa kwenda Makongorosi na kuiomba serikali kutenga fedha ili ikamilike na hivyo kufungua fursa za uchumi katika mikoa yao.
“Kwenye wilaya yetu ya Ikungi kuna barabara inaitwa Ikungi,Mang’onyi mpaka Kilimatinde, barabara hii ni ya kiuchumi kuna kampuni kubwa za madini zitalipa kodi,hivyo niombe barabara hii iangaliwe namna ya kuwekewa lami ili iongeze fursa za uchumi katika eneo letu,
“Nikumbushe pia barabara ya wenzetu ya Bulyanhulu – Kahama yenye kilomita 61,hii ikiwekwa lami kwa sababu kodi tunapata nyingi kupitia madini itasaidia kuongeza uchumi wan chi yetu,tukumbuke barabara ni muhimu ,miundombinu ni muhimu naomba serikali iweze kujenga barabara za lami ili kuongeza uchumi wetu,”amesisitiza.
MWISHO.