Mkuu wa Kitengo cha Ubunifu wa Benki ya NMB, Josina Njambi akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi rasmi wa tamasha la Wiki ya Ubunifu (Innovation Week) iliyoanzishwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) na wadau mbalimbali. Benki ya NMB ni mdhamini wa wiki hiyo ya ubunifu.
******************************
Na Mwandishi Wetu,
BENKI ya NMB imeazimia kufungua fursa zaidi kwa wateja wake kupitia huduma mbalimbali zinazoendana na mabadiliko ya kiteknolojia ili kurahisisha upatikanaji huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya wiki ya ubunifu ambapo NMB ni sehemu ya wadhamini jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Ubunifu kutoka benki hiyo, Bi. Josina Njambi alisema lengo la kuwa sehemu ya tukio hilo ni kutaka kujivuta karibu zaidi na wadau wanaojihusisha na ubunifu.
Alisema, Benki ya NMB ni miongoni mwa benki kubwa nchini iliyokuwa ya mwanzoni kutumia ubunifu kuwapa wateja huduma wanazostahiki ikiwemo huduma ya NMB Mkononi.
“Tulipunguza mlolongo wa wateja kupanga foleni kwenye matawi yetu kwa kutoa huduma ya benki kwa simu za mkononi, tulipunguza mlolongo kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) kwa kuanzisha NMB Wakala nchi nzima, huu ni ubunifu wa kipekee tuliopata kuufanya,” alisema Bi. Njambi.
Aidha, aliweka wazi kuwa kila siku wanafikiria namna ya kumthamini mteja wao kwa kuwa wabunifu zaidi, ambapo alieleza kuwa ubunifu unasaida vilevile kuongeza ajira kwa vijana na watanzania wote kwa ujumla kupitia utoaji huduma.
“Ndiyo maana tulitangaza shindano la kupata vijana watakaokuja na ubunifu wa kipekee kwenye huduma ya NMB Mkononi, ambapo tayari tumeshapata vijana 15 watakaoanza kuchuana kwa siku nne kuanzia kesho Jumanne hadi Ijumaa wiki hii. Mshindi atapata Shilingi Milioni 1. Tunachotaka ni kuona kikundi gani kitakuja na utaalamu wa kipekee kwenye ubunifu wa kupata app na huduma zingine za NMB zilizo kidijitaliii zaidi kwa manufaa ya wateja wetu ili wapate urahisi zaidi katika kufanya miamala popote walipo na wakati wowote,” alieleza Bi. Njambi.
Awali, katika tamasha la Wiki ya Ubunifu (Innovation Week) iliyoanzishwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Tanzania Commission for Science and Technology – Costech) washiriki walieleza mambo mbalimbali juu ya safari yao katika ubunifu hasa vijana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Costech, Dk. Amos Nungu alisema awali wazo lilikuwa ndani ya tume hiyo lakini baadae wadau wakaamua liwe wazo la nchi nzima kwa kuwa kila kijana wa Kitanzania anahitaji kunufaika na ubuifu.
“”Tunafahamu kuwa kazi ya serikali ni kuweka mazingira wezeshi, sisi taasisi nyingine tunatakiwa kuzitumia fursa zinazoletwa na serikali kunufaika na kufanya mambo ya kiubunifu hasa katika zama hizi za Sayansi na Teknolojia,” alisema Dk. Nungu.
Aidha, mmoja wa watoa mada Dk. Flora Ismail Tibarazwa ambaye ni Mkurugenzi wa Programu ya Kusaidia Ubunifu kwa nchi za Ukanda wa Kusini: Southern African Innovation Support Programme (SAIS) alisema ubunifu ni miongoni mwa vyombo vinavyotoa suluhu ya tatizo la ajira duniani na hasa bara la Afrika.
“Uchumi unakua kupitia ubunifu, lakini pia unatoa suluhu ya tatizo la ajira na kujiajiri kwa vijana, wawekezaji pia wanapata uwanja mpana wa kusaidia jamii katika maeneo wanayotaka kuanzisha biashara zao,” alisema Dk. Tibarazwa.
Kwa mwaka huu tamasha hilo lenye kaulimbiu ‘Innovation for a Resilient and Inclusive Digital Economy’ ambapo kwa Kiswahili linasomeka: “Ubunifu kwa Uchumi wa Kidijitali Stahimilivu na Jumuishi” limetimiza miaka saba tangu liwe la kitaifa lakini pia limesaidia kufungua fursa nyingi kwa vijana.