Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula
TANZANIA YAZINDUA RASMI MAADHIMISHO YA MIAKA 40 YA SADC
Na Mwandishi wetu, Dar
Tanzania imezindua rasmi maadhimisho ya kitaifa ya Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tarehe 1 Aprili 1980.
Akiongea kuhusu uzinduzi wa maadhimisho hayo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi 16 za SADC imejipanga kikamilifu kuadhimisha miaka 40 ya SADC. Pamoja na maadhimisho hayo, Jumuiya imepata mafanikio kadhaa tangu kuanzishwa kwake pia mafanikio hayo yanalenga kufanikisha masuala ya kuenzi mchango mkubwa wa Viongozi Wakuu waanzilishi wa SADC ambao maono yao yaliweka msingi wa ukombozi wa kisiasa na kiuchumi kwa Kanda ya Kusini mwa Afrika.
“Pamoja na mambo mengine, tumejipanga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mtangamano wa SADC na faida za uanachama kwenye Jumuiya hii ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo za kiuchumi, kijamii na kisiasa, kuangazia mafanikio yaliyofikiwa katika masuala ya amani na usalama na pia maendeleo ya kiuchumi kwa watu wote katika Kanda ya Kusini mwa Afrika; na kuongeza hamasa kwa makundi mbalimbali kama wafanyabiashara, vijana, wanawake, makundi maalum na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zinazopatikana kupitia uanachama wa SADC,” amesema Balozi Mulamula.
Waziri Mulamula ameongeza kuwa, katika kusherehekea maadhimisho hayo , Tanzania imejipanga kuandaa mihadhara kuhusu umuhimu wa SADC kwa Tanzania na Kanda ya Kusini mwa Afrika kwa ujumla. Mihadhara hiyo itafanyika katika baadhi ya vyuo vikuu hapa nchini. Tarehe 21 Mei, 2021, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) utafanyika tarehe 19 Mei, 2021 na mhadhara katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) utafanyika tarehe 26 Mei 2021 pamoja na mhadhara wa hitimisho utafanyika tarehe 27 Mei, 2021 katika Chuo cha Diplomasia (CFR). kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
“Itakumbukukwa kuwa, Tanzania wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ilifanya kazi kubwa ya kusaidia harakati za ukombozi hususan kwa nchi za Kusini mwa Afrika. Kadhalika, Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilikuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2018 hadi Agosti 2019 ambapo katika kipindi hicho cha uenyekiti mchango wa Tanzania ulifanikisha masuala mbalimbali ndani ya SADC kukamilika ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa hali ya Ulinzi na Usalama na masuala ya demokrasia na utawala bora katika nchi za SADC,” amesema Waziri Mulamula
Balozi Mulamula ameyataja mafanikio mengine ni pamoja na kuzinduliwa kwa mfumo wa uombaji na utoaji vyeti vya utambuzi wa Uasili wa Bidhaa kwa njia ya mtandao, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara la SADC, kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa SADC wa megawati 3,595 sawa na asilimia 90 ya lengo la kuzalisha megawati 4000, kuandaliwa kwa Dira ya maendeleo ya SADC ya mwaka 2050 pamoja na Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda (RISDP) wa Mwaka 2020-2030.
“Mafanikio mengine ni kuridhiwa kwa lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne za SADC, kupitishwa kwa Azimio la Kuondolewa Vikwazo vya iuchumi vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe tangu mwaka 2000. Azimio hilo liliridhia tarehe 25 Oktoba ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kupinga vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe,” amesema Balozi Mulamula.
Aprili 1980, Mkutano wa Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Coordination Conference-SADCC) (SADCC) ilianzishwa rasmi huko Lusaka, Zambia baada ya Nchi za Mstari wa Mbele kuridhia Azimio la Lusaka lililojulikana kama “Kusini mwa Afrika: Kuelekea Ukombozi wa Kiuchumi ambapo pamoja na mambo mengine, ulilenga kuimarisha sekta muhimu za kuchochea maendeleo ya kanda kama vile Uchukuzi na Mawasiliano, Kilimo na Chakula, Viwanda, Maendeleo ya Rasilimali Watu na Nishati. Nchi Wanachama waanzilishi wa SADCC ni Angola, Botswana, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Agosti 1992, jijini Windhoek, Namibia Wakuu wa Nchi na Serikali walisaini Mkataba wa kuibadilisha SADCC kuwa SADC. Hatua hii ilitoa fursa ya kutafsiri upya misingi ya ushirikiano miongoni mwa Nchi Wanachama kutoka kwenye muungano usio rasmi na kuwa muungano wa kisheria. Hadi sasa, SADC ina wanachama 16 ambao ni Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Ushelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Aidha, kumbukumbu ya maadhimisho hayo kwa ngazi ya kikanda itahitimishwa tarehe 5 Juni, 2021 kwa mhadhara wa umma utakaofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Mei hadi 8 Juni 2021 Maputo, Msumbiji.
Kaulimbiu ya maadhimisho haya ni: “Miaka 40 ya SADC ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahimilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia”