**************************************
Na Mwandishi wetu, Babati
WAKAZI wa Mkoa wa Manyara, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Charles Makongoro Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere kuwa Mkuu mpya wa Mkoa huo.
Wakazi hao wamedai kuwa hayati Nyerere ana historia kubwa mkoani Manyara tangu enzi ya kudai uhuru hivyo ni heshima kubwa kwao kupatiwa Makongoro ili awaongoze.
Kada maarufu wa CCM Mkoani Manyara, Cosmas Masauda amesema machifu wa kutoka mkoa huo, Chief Herman Sarwat na Chief Amiri Dodo walimsaidia mwalimu Nyerere kudai uhuru hivyo Makongoro amerudi nyumbani.
Masauda amesema hata nyumba aliyokuwa anafikia hayati mwalimu Nyerere bado ipo mbele ya mlima Kwaraa mjini Babati hivyo wamefurahia kuongozwa na mtoto huyo wa Rais wa awamu ya kwanza.
“Manyara ni mkoa unaoamini kwenye utamaduni hivyo wazee wa kimila wamejiandaa kumpokea Mkuu mpya wa Mkoa huu Makongoro na kumfanyia tambiko la kimila ili kumkaribisha,” amesema Masauda.
Amesema Makongoro ni mtu mwenye historia nzuri kwani hana matukio ya ufisadi na amerithi uzalendo wa baba yake hayati mwalimu Nyerere katika kuipenda nchi yake hivyo wana imani naye.
Amesema wananchi wa mkoa wa Manyara wana matumaini makubwa kwa Makongoro ili azidi kuwaunganisha wakulima na wafugaji ambayo ni jamii kubwa zilizopo kwenye eneo hilo.
“Wananchi wa mkoa wa Manyara watampa ushirikiano wa kutosha kwani walikuwa wanampenda hayati mwalimu Nyerere na Makongoro wanampenda pia,” amesema Masauda.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirikia mkoani Manyara, Venance Msafiri amesema wanamkaribisha mkuu mpya wa mkoa huo Makongoro ili kuendeleza maendeleo yaliyopo.
Msafiri amesema anaamini Makongoro ataendeleza mema yote yaliyofanywa na watangulizi wake wa awali waliowahi kuongoza kwenye Mkoa wa Manyara.
Amesema wanamshukuru Mungu bado Rais Samia ameendelea kumuamini Mkirikiti na kumpangia kituo kingine cha kazi kwenye Mkoa wa Rukwa ambapo anaamini ataendelea kufanya kazi vyema.
Mkazi wa eneo la Kwere Mohamed Issa amesema watashirikiana na Makongoro kuhakikisha Manyara inasonga mbele na kufikia hatua nyingine zaidi ya hapo ilipo.