*********************************
LEO Mei 12, 2021, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote duniani kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani.
Siku hii ya kimataifa ilitangazwa na kuzinduliwa rasmi mwaka 1992. Lengo la kuwepo kwa siku hii ni kuwatambua na kuwapongeza wauguzi kwa mchango wao muhimu katika jamii. Siku hii pia inatoa fursa kwa wauguzi kote duniani kutafakari mahali walipo na kule waendako katika kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma. Aidha, ni nafasi ya kubainisha pale ambapo kumeonekana upungufu katika utendaji ili paweze kurekebishwa.
Tume inatambua umuhimu na mchango mkubwa wa wauguzi katika jamii, na hili linadhihirishwa na uwepo wao kutoka ngazi ya chini kabisa ya huduma za afya hadi ngazi za juu, kwa maana nyingine kila alipo mgonjwa, muuguzi yupo.
Tume inapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wauguzi wote nchini kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya katika kujenga na kuendeleza taifa letu.
Tume inaipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa hivi karibuni wa kuajiri watumishi 2,726 wa kada mbalimbali katika sekta ya afya na kwa dhamira yake ya kuboresha miundombinu ya sekta ya afya kwa kujenga kituo cha afya katika kila Kata na zahanati katika kila Kijiji. Pia Tume inaipongeza Serikali kwa kuruhusu uwepo wa vyombo vinavyotetea maslahi ya wauguzi, ikiwemo Baraza la Wauguzi na vyama vya wafanyakazi.
Ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu ni: “Wauguzi sauti inayoongoza, Dira ya huduma ya afya”. Ujumbe huu unabainisha umuhimu wa wauguzi katika kufikiwa kwa dira ya huduma ya afya kwa wananchi wote, kwani bila wauguzi litakuwa ni jambo la kufikirika kuifikia dira hiyo.
Pamoja na umuhimu wa kada hii hapa nchini, wauguzi wanakabiliwa na changamoto nyingi; ikiwemo: Uchache wa wauguzi, kutukanwa, kukashifiwa na mara nyingine kupigwa na ndugu wa wagonjwa wanaowahudumia, uhaba wa vifaa na vitendea kazi, msongamano wa wagonjwa kwenye vituo vya afya, na uhaba wa fursa za kujiendeleza kielimu. Tume inaamini changamoto hizi zinaweza kuondoshwa kwa wadau wote ndani na nje ya nchi kushirikiana pamoja na kudhamiria kuziondosha.
Kwa upande mwingine utendaji wa wauguzi unaathiriwa na ongezeko la uvunjwaji wa maadili ya kitaaluma katika kazi za wauguzi, kwani vipo visa na malalamiko dhidi ya baadhi ya wauguzi; ikiwemo rushwa, kuvujisha siri za wagonjwa na matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa.
Hivyo tunapoadhimisha siku hii muhimu, Tume inapenda kutoa wito ufuatao kwa wadau:
- Serikali iendelee kuwekeza zaidi katika tasnia ya uuguzi ili wapatikane wauguzi wengi zaidi ili kupunguza nakisi ya wauguzi nchini.
- Serikali iendelee kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwaendeleza wauguzi kitaaluma.
- Serikali iendelee kuweka mazingira bora na salama ya kufanyia kazi, ikiwemo kuboresha maslahi ya wauguzi.
- Wauguzi wazingatie maadili ya kitaaluma na kuwajibika licha ya changamoto zinazowakabili.
- Wauguzi na watendaji wengine katika sekta ya afya wahakikishe kuwa haki za binadamu zinazingatiwa katika utoaji wa huduma za afya na watambue kuwa kila mtu anayo haki ya kupata huduma ya afya bila kujali jinsia, kabila na nafasi yake katika jamii.
- Wananchi wajiepushe na vitendo vinavyoweza kuwavunja moyo wauguzi na watoa huduma ya afya, ikiwemo lugha chafu na kujichukulia sheria mkononi.
Imetolewa na: