Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akichangia bajeti ya Wizara ya Afya bungeni jijini Dodoma
MBUNGE
wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina amewataka wabunge kutopitisha
Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
hadi suala la wizi wa dawa litakapotafutiwa ufumbuzi kwani limeleta
madhara na malalamiko makubwa kwa wananachi kukosa dawa kwenye vituo
vya Serikali vya kutolea huduma.
Akichangia
hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kwa mwaka 2021/2022, Mpina amesema katika hotuba ya Waziri wa Afya, Dk.
Dorothy Gwajima imetaja kuwepo tatizo la wizi wa dawa lakini Serikali
haijaonesha ni kwa namna gani tatizo hilo lilivyo kubwa na hatua
zilizochukuliwa kwa wezi hao wa dawa za wananchi.
“Mh.
Naibu Spika nimesoma hotuba ya Waziri kuhusu suala hili nadhani iko
ukurasa wa 61 lakini Mh Naibu Spika suala hili la wizi wa dawa
linavyoripotiwa ni kubwa sana lakini nimeona kwenye hotuba ya waziri
pale ni kama imeandikwa kama para moja hivi nataka niseme hivi kwa ufupi
kwamba tatizo hili ni kubwa” amesema Mpina.
Mpina
amesema Waziri wa Afya aliwahi kutangaza vita dhidi ya wezi wa dawa
lakini dawa zimeibiwa Songwe ambapo alitangaza Waziri mwenyewe kuwa dawa
zenye thamani ya milioni 13.5 ziliibiwa lakini pia Ukerewe dawa za
milioni 200 ziliibiwa na kwenye taarifa yake anakiri kwamba wizi huo
unasababisha huduma za dawa zisiwafikie wananchi.
“Sasa
hivi kweli leo hii Serikali imeshindwa kabisa kudhibiti hawa wezi wa
dawa? Mpaka leo wanaendelea kuiba dawa? Nani anayeiba dawa hizi?
anafanikiwaje kuiba dawa katika Serikali ambayo imejipanga kuanzia
kwenye kitongoji, kwenye kijiji, kwenye kata , kwenye tarafa, kwenye
wilaya, na ina vyombo vya dola kila sehemu hawa wezi wa dawa ni akina
nani ambao hawawezi kukamatwa na kuadhibiwa” anasema Mpina
Mpina
amesema kwenye taarifa ya Waziri angetuambia amekamata wezi wangapi
toka ainze vita dhidi ya wezi wa dawa lakini hakuna, Nani ameiba dawa?
anafanikiwaje kuiba dawa na dawa hizi zinaibiwa zinakwenda kuuzwa wapi?
nani ananunua dawa hizi, mtandao wa wizi huo nani anaufadhili mpaka
kiasi kwamba tushindwe kukomesha suala hili.
“Sasa
watu wanaiba dawa leo tunaenda kuidhinisha bajeti ya dawa zikaibiwe ni
shida sana kupitisha bajeti ya waziri huyu ambaye yeye mwenyewe anakiri
kwamba kutokana na wizi huu dawa haziwafikii wagonjwa sasa kama dawa
haziwafikii wagonjwa Bunge hili lijishirikishe kikamilifu kuhakikisha
kwamba kwanza tunamaliza tatizo la wizi wa dawa halafu ndio tupitishe
bajeti” Mpina.
Mpina amesema bila kumaliza tatizo hilo la wizi wa dawa itakuwa ni tunawaongopea watanzania kuhusu suala hili la wizi wa dawa.
“Mh.
Naibu Spika ukisoma kiambatisho cha sita ambacho Waziri amekisema yeye
mwenyewe ukisoma yale matukio ukiukwaji mkubwa wa manunuzi watu
wananunua dawa wanavyotaka wenyewe, watu wameiba dawa, watu wamefanya
kila aina ya hujuma hatua kwa nini hazichukuliwi? Kwanini hatuambiwi “
alihoji Mpina
Mpina
amesema ilitakiwa Serikali ije na mkakati mahususi wa kumaliza tatizo
la wizi wa dawa kwa kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya dawa.
“Tulitegemea
wezi wa dawa hawa tungekutana nao kila siku wana pingu mkononi kila
kunapokucha, Serikali hii haiwezi kushindwa kudhibiti wezi wa dawa,
tumeweza ufisadi, tumeweza uvuvi haramu, tumeweza hayo, tumeweza madawa
ya kulevya leo hii tunakuja kushindwaje suala la wizi wa dawa kuna mtu
hapa hajawajibika sawa sawa Mh Naibu Spika” amesema Mpina