Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano wa Watendaji wa Sekta ya Maji kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma, Mei 11, 2021.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Watendaji wa Sekta ya Maji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma, Mei 11, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa malori matatu ya kunyonya majitaka ambayo aliyakabidhi kwa Halmashauri za Miji ya Kahama, Tanga na Lindi baada ya Waziri Mkuu kuhutubia Mkutano wa Watendaji wa Sekta ya Maji kwenye ukumbi wa Chuo hicho jijini Dodoma, Mei 11, 2021. Wengine pichani kutoka kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, William Tate Ole Nasha na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandishi Anthony Sanga.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa pili kulia) wakikagua pikipiki 147 ambazo zimenunuliwa na Wizara ya Maji na zimekabidhiwa kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Ukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma baada ya Waziri Mkuu kuhutubia Mkutano wa Watendaji wa Sekta ya Maji Mei 11, 2921.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (aliyepanda pikipiki) baada ya kukabidhi pikipiki 147 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) kwenye viwanja vya Ukumbi wa Chuo cha Mpiango jijini Dodoma ambako pia alihutubia Mkutano wa Watendaji wa Sekta ya Maji, Mei 11, 2021.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
.……………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wote wa sekta ya maji nchini kufanya kazi kwa uzalendo, bidii na weledi na kwa kutanguliza maslahi mapana ya nchi.
Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji nchini kinaongezeka ili kufikia malengo ya kufikisha maji kwa kiwango cha asilimia 85 Vijijini na asilimia 95 Mijini ifikapo mwaka 2025.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Mei 11, 2021) wakati wa mkutano wa watendaji wa sekta ya maji uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa sekta maji nchini kushirikiana na wanajiosayansi kufanya tafiti za mara kwa mara zitakazotuwezesha kuwa na takwimu za uhakika kuhusu kiwango cha maji, mahali yalipo na ujazo wake.
“Kama nilivyotangulia kueleza kuwa maji ni chachu katika maendeleo ya viwanda nchini. Kwa mantiki hiyo, uwepo wa takwimu sahihi kuhusu upatikanaji wa maji ni muhimu katika kurahisisha na kuvutia uwekezaji wa viwanda kote nchini”
Aidha, Waziri Mkuu ameigiza Wizara ya Maji ishirikiane na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kusimamia vema na kwa uadilifu rasilimali fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ili miradi iweze kukamilika kwa wakati na uwepo wa thamani ya fedha za walipa kodi.
Akizungumzia kuhusu uboreshwaji wa huduma ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi waishio vijijini na mijini, Waziri Mkuu amesema “kufikia Machi 2021, jumla ya miradi 177 ya maji imeendelea kutekelezwa katika Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya, Miji midogo na Miradi ya Kitaifa. Tayari, miradi 67 imekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 759.211 na utekelezaji wa miradi 110 upo katika hatua mbalimbali”
Waziri Mkuu pia alikabidhi pikipiki 147 kwa ajili ya mameneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Viijini, malori matatu ya kunyonya majitaka kwa halmashauri za miji ya Kahama, Tanga na Lindi.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa hatakuwa na huruma na mtendaji yeyote atakayegundulika anahujumu miradi ya maji, lengo ni kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama wakati wote.
Amesema “Hatuwezi kukubali wakandarasi wasio na uwezo wa kufanya kazi, tutawapa kazi wakandarasi wenye uwezo wa kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji”
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Ummy Mwalimu amesema kuwa ataweka mazingira rafiki kwa RUWASA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuhakikisha miradi yote maji inakamilika.