………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI mstaafu wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Clempu Ole Kinoka ameshinda kesi na kurudishiwa shamba lake la zaidi ya ekari 1,000 lililopo mpakani mwa Kijiji cha Langai na Naberera.
Clempu ameshinda kesi hiyo iliyokuwa kwenye mahakama Kuu ya Mkoa wa Arusha, dhidi ya mfugaji Lenginyu Yamat.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imeagiza Lenginyu aachalie shamba hilo mara moja na kulipa faini ya shilingi milioni 120.
Klempu ameishukuru Mahakama hiyo kwa kutoa haki yake kwani shamba hilo alipata kihalali kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Amesema mgogoro kwenye shamba hilo ulianza tangu mwaka 2019 na baadhi ya wanasiasa walichochea ili waichukue ardhi hiyo.
“Namshukuru Mungu nimefanikiwa kupata tena shamba langu ambalo nilinunua kwa njia ya halali kwa kufuata sheria tangu awali,” amesema Clempu.
Mfanyabiashara wa Naisinyai, Siria Ngodedia amesema anamshukuru Mungu kwani Mahakama imetenda haki na kurejesha ardhi hiyo kwa Diwani huyo mstaafu.
“Haki ya mtu haiwezi kwenda bure, Mahakama imeona mahali haki inapaswa kuwepo, tunamshukuru Mungu kwa hilo kwani mzee amerudishiwa eneo lake na kazi iendelee,” amesema Siria.
Mkazi wa kijiji cha Langai, Ernest Martini amesema siasa chafu ilitaka kutumika ili kumdhulumu Clempu eneo lake kwani alinunua kihalali shamba hilo.
“Baadhi ya viongozi walitumika vibaya na kutaka kudhulumu mali ya Diwani huyo mstaafu wa kata ya Naisinyai ila Mahakama imetenda haki,” amesema.