…………………………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza.
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limeshua (limezindua) Mfumo wa Elimu Masafa (Bakwata Online Academy) ili kuwajengea uwezo na weledi viongozi wa Dini ya Kiislamu wa ngazi mbalimbali kusoma kozi ya uongozi,utawala bora na TEHAMA.
Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli, alizindua mfumo jana kwenye Ukumbi wa Makumbusho wa Hoteli ya New Mwanza,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Mongella, akisema BAKWATA kuzindua mfumo wa Elimu Masafa ni jambo kubwalenye tija litatoa ajira, kurahisisha biashara mtandao na kupunguza umbali wa kutembea kwa watakaojiunga na mafunzo hayo.
Alimshukuru Mufti Sheikh Abubakar Zuberi Mbwana kwa kazi ya kulingania Uislamu na kuufanya ukimbie badala ya kutembea kwamba Bakwata huko nyuma kulikuwa na mifarakano,leo kuna mshikamno hata Mwanza imesimama na imekuwa kiungo baina ya serikali.
“Miradi ya Bakwata sasa inatembea,leo mmefikiria kuanzisha chuo (shule) kupitia kwa Mufti, sasa kufungua Bakwata Online Academy,rai yangu itumieni vizuri ili kuelimika sababu mtandao huo una faida kubwa kuliko hasara lakini mkiutumia vibaya utawaharibu,”alisema Mogella.
Alisema hata serikali inatumia mfumo huo kwenye Chuo Kikuu Huria (OUT) na akawataka waislamu wengi kujiunga na kutumia mtandao huo kujielimisha kwa weledi, kufanya biashara, kuhifadhi taarifa na kumbukumbu muhimu.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwaomba viongozi wa Bakwata kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kujipambanua kwake na jinsi anavyowaunganisha Watanzania, waondoe mifarakano na migogoro kwa serikali iko tayari kupokea ushauri watakaoutoa.
Alisistiza yapo mambo wamejifunza kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhani wasiayache baada ya mfungo kumalizika bali waendelee nayo kwa kuzingatia nguzo tano za uislamu ili kuwafanya wasio waislamu waupende hivyo wanapaswa kuwa watu wa heri wakizingatia uislamu ni heshima na hekima.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata taifa, Sheikh Hamis Mattaka, alisema Bakwata ni chombo kinachopokea viongozi wenye sifa na uzoefu mbalimbali wanaoteuliwa na jamii, kuashua mpango huo wa Bakwata Online Academy kunabeba falsafa ya Mufti ya kusaidia umma wa waislamu na hautamwacha kiongozi yeyote nje.
“Mheshimiwa Mufti aliliona baraza na kuamua kuanzisha hiki kimataifa ukiwa mchakato wa kusahihisha mambo yenye mapungufu sababu lilijikuta likipokea watu wasio na uwezo, wakipewa elimu watajua namna ya kuongoza bila kuwakwaza kwenye kazi zao na elimu hiyo kiwe kigezo cha uongozi.
Aidha Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, alitoa wito kwa viongozi na waislamu wasio viongozi,watumie fursa ya elimu masafa ndio mwarobaini wa migogoro, itawawezesha kiuchumi, kibiashara na kuwasiliana sababu wengi hawana uelewa wa utendaji, utawala na ufahamu wa katiba.